Rouhani: Umoja na kujituma, ufunguo wa kusimama kidete dhidi ya maadui
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i62099-rouhani_umoja_na_kujituma_ufunguo_wa_kusimama_kidete_dhidi_ya_maadui
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema umoja na jitihada ni mambo mawili ambayo yamefanikisha muqawama wa taifa hili dhidi ya maadui.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 09, 2020 11:00 UTC
  • Rouhani: Umoja na kujituma, ufunguo wa kusimama kidete dhidi ya maadui

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema umoja na jitihada ni mambo mawili ambayo yamefanikisha muqawama wa taifa hili dhidi ya maadui.

Rais Rouhani amesema hayo leo Alkhamisi wakati wa hafla ya uzinduzi wa miradi mikubwa ya viwanda na nishati katika mikoa ya Sistan na Baluchestan, Fars na Isfahan na kuongeza kuwa, umoja na kufanya bidii ni ufunguo wa kusimama kidete dhidi ya maadui.

Amesema Marekani inataka kuitumbukiza Iran katika mgogoro wa kiuchumi kwa kuvuruga soko la fedha za kigeni hapa nchini.

Dakta Rouhani ameeleza bayana kuwa, wananchi wa Iran wataendelea kushuhudia kupigwa hatua za ustawi na maendeleo mwaka huu, licha ya janga la corona na mashinikizo ya maadui wa taifa hili.

Rais Rouhani katika uzinduzi wa miradi ya maendeleo uliofanyika kwa njia ya intaneti

Rais wa Iran amesema njama za maadui ni kutaka kuipa Iran pigo kupitia mashinikizo, kuvunja matumaini ya wananchi na kuibua mifarakano baina ya wananchi na viongozi. Hata hivyo amesisitiza kuwa, kutokana na kusimama kidete taifa hili, njama hizo za maadui zitagonga mwamba.

Ameongeza kuwa, "mwaka huu, miradi mikubwa 200 ya viwanda na madini yenye thamani ya Tomani bilioni 170,000 za Iran itazinduliwa humu nchini. Miradi hiyo itaendelea kuzinduliwa hatua kwa hatua katika wiki za hivi karibuni licha ya changamoto zilizopo."