Rouhani: Iran itaendelea kustawi pamoja na kuwepo vizingiti vya maadui
Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema taifa la Iran litaendelea kustawi pamoja na kuwepo zivingiti ambavyo vinawekwa na maadui.
Rais Rouhani ameyasema hayo leo Alhamisi alipokuwa akihitubu kwa njia ya video baada ya kuzindua miradi ya viwanda na uchimbaji madini katika mikoa ya Mazandaran, Khuzestan na Fars. Rouhani amesema katika mazingira magumu ambayo adui ameyzibua dhidi ya Iran, taifa hili limeweza kustahamili vikwazo na pia janga la corona.
Aidha amesema mwaka huu pekee, tani milioni 26 zitaongezwa katika uzalishaji wa chuma nchini Iran na nukta hiyo inaonyesha kustawi sekta ya uzalishaji kiviwanda nchini.
Katika hotuba yake, Rais Rouhani kwa mara nyigine ametoa wito kwa wananchi kuzingatia kanuni za kiafya ili kuzuia kuenea ugonjwa wa corona. Aidha amewapongeza wafanyakazi wa sekta ya afya kutokana na jitihada zao katika zama hizi za jana la corona.
Amesema janga la corona limevuruga vibaya baadhi ya ajira na hivyo kuna haja ya kutekelezwa mikakati ya kubuni nafasi mpya za ajira.
Rais Rouhani ametoa wito kwa sekta binafsi na za umma kushirikiana kutatua matatizo ya wananchi ili kumkatisha tamaa adui.