Mfumo wa ubeberu wa Marekani; mfumo unaochukiwa zaidi duniani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i62606-mfumo_wa_ubeberu_wa_marekani_mfumo_unaochukiwa_zaidi_duniani
Mfumo wa ubeberu wa Marekani ndio mfumo unaochukiwa zaidi duniani kwa sababu, kutokana na kiwango cha juu zaidi cha chuki ulizoeneza ndani ya nyoyo za watu wa mataifa mbali mbali ulimwenguni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 04, 2020 03:03 UTC
  • Mfumo wa ubeberu wa Marekani; mfumo unaochukiwa zaidi duniani

Mfumo wa ubeberu wa Marekani ndio mfumo unaochukiwa zaidi duniani kwa sababu, kutokana na kiwango cha juu zaidi cha chuki ulizoeneza ndani ya nyoyo za watu wa mataifa mbali mbali ulimwenguni.

Hayo yameelezwa na Sayyid Ibrahim Raisi, Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran katika kikao cha jana Jumatatu cha Baraza Kuu la wakuu wa idara hiyo.

Raisi aliashiria chokochoko za mfumo wa ubeberu za kuibua changamoto dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na akasema: Wamarekani ambao kwa miaka mingi wamekuwa vinara wa dhulma na ukiukaji wa haki za binadamu katika maeneo mbalimbali ya dunia sasa wao wenyewe wamekumbwa na maovu hayo ya dhulma na ukiukaji wa haki za binadamu, lakini bado wanaendeleza mienendo ya kihasama dhidi ya mataifa mbalimbali. 

Ayatullah Sayyid Ibrahim Raisi, Mkuu wa Idara ya Mahakama

Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vilevile amevipongeza vikosi vya usalama kwa kumtia nguvuni kinara wa genge la kigaidi la Tondar na akasema: Nchi zinazodai kutetea haki za binadamu sasa zimekuwa maficho salama ya magaidi; na Marekani na nchi za Ulaya zinawalea na kuwapa misaada magaidi wa makundi yanayofanya mauaji ya kutisha dhidi ya watu wasio na hatia katika pembe mbalimbali za dunia.

Hali ya kusikitisha ya vita na umwagaji damu inayoshuhudiwa kwa miaka kadhaa sasa katika nchi za Afghanistan, Iraq na Yemen pamoja na uvamizi na mauaji yanayofanywa na tawala zinazoteketeza roho za watoto wadogo huko Palestina na Yemen kwa uungaji mkono wa Marekani, ambazo ni dhulma zinazofanywa na Washington dhidi ya mataifa yanayongeshwa ni kielelezo cha wazi cha ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na mfumo wa ubeberu duniani. Dhulma kubwa zaidi katika karne za karibuni ni ile iliyofanywa katika ardhi ya Palestina. Katika dhulma hiyo yenye kuungulisha nyoyo, watu hawakuporwa ardhi yao tu lakini walipokwa na kunyang'anywa pia hata utambulisho wao. Kuna mifano mingi inayodhihirisha uzandiki na undumakuwili wa Magharibi katika suala la haki za binadamu. Kwani hata ndani ya nchi hizo pia raia wengi wanateseka kutokana na ubaguzi wa rangi, dhulma na ufisadi, kiasi kwamba mayowe ya kulalamikia dhulma hizo yanazidi kusikika kwa sauti ya juu zaidi siku baada ya siku. Wimbi kubwa la malalamiko hayo limedhihiri kitambo kidogo tu nyuma ndani ya Marekani baada ya askari polisi mzungu kumuua kikatili raia mmoja mweusi. Na licha ya ukandamizaji mkubwa uliofanywa na vyombo vya dola kwa lengo la kuzima malalamiko hayo, maandamano makubwa yangali yanaendelea kushuhudiwa nchini humo.

Maandamano ya kulalamikia ubaguzi wa rangi Marekani

Katika sehemu moja ya ujumbe aliotoa hivi karibuni kwa mnasaba wa siku za Hija, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, aliashiria sura na malengo ya mwenendo wa kinyama na usio wa kiutu wa Marekani na akabainisha kwamba:

Muamala wa Marekani kwa mataifa dhaifu ni taswira pana ya mwenendo wa yule askari polisi aliyemwekea goti la shingo mtu mweusi asiyeweza kujihami na akambinya mpaka akafika hadi ya kukata roho.

Fedheha iliyowapata viongozi wa Ikulu ya White House kutokana na mienendo yao isiyo ya kibinadamu hivi sasa imedhihirika kwa mayowe yanayopigwa na wananchi wanaoandamana kwenye barabara na mitaa ya Marekani.

Fouad Izadi, mtaalamu wa Mahusiano ya Kimataifa anasema, ni zaidi ya nusu karne sasa suala la "haki za binadamu" limekuwa likitumiwa kama wenzo wa mashinikizo na Marekani dhidi ya maadui na washindani wa nchi hiyo. Akifafanua zaidi nukta hiyo, msomi huyo anasema:

Marekani, ambayo inadai kuwa inatetea haki za binadamu, haiwafanyii vitendo vilivyo dhidi ya haki za binadamu raia wa nchi zingine tu, bali inawakandamiza pia hata raia zake yenyewe. Kwa kweli tunaweza kusema, wahanga na waathirika wa mwanzo kabisa wa haki za binadamu za Kimarekani ni Wamarekani wenyewe. Tunashuhudia katika kurasa za historia ni jinsi gani Wahindi Wekundu waliovyouliwa kwa halaiki; na Wamarekani weusi walivyofanywa watumwa. Haya yote yanaonyesha kuwa ndani ya mipaka ya Marekani pia, raia wa nchi hiyo hawajasalimika na sera za haki za binadamu za Kimarekani kutokana na kuandamawa na mashinikizo makali ya siasa zilizo dhidi ya haki za binadamu za nchi hiyo.

Watu weusi waliogeuzwa watumwa na kutumikishwa mashambani nchini Marekani

Marekani imejaribu kutumia pia vikwazo vya dawa katika kipindi hiki kigumu kinachotokana na mripuko wa janga la corona ili kuyafanya maisha ya wananchi wa Iran yawe ya tabu na dhiki. Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya zinazojinasibu kuwa ni watetezi wa haki za binadamu ziliuunga mkono utawala wa Saddam wakati wa vita vya kulazimishwa, ulivyoanzisha dhidi ya Iran kwa kuupatia silaha za kemikali ulizotumia kuwashambulia raia wa Iran. Matokeo ya uungaji mkono huo yalikuwa ni kuteketea roho za watu zaidi ya laki moja waliofanywa mhanga wa silaha za kemikali alizotunukiwa Saddam na Magharibi.

Kama vile haitoshi, Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya zimekuwa zikiliunga mkono genge la kigaidi la Munafiqina (MKO) pamoja na makundi mengine ya kigaidi ambayo yamewaua shahidi maelfu ya watu wasio na hatia nchini Iran. Faili chafu la haki za binadamu la Marekani limejaa pia madoa meusi ya jinai ilizofanya katika magereza ya Guantanamo na Abu Ghuraib. Pamoja na yote hayo nchi hizo zinajigamba kuwa ni watetezi wa haki za binadamu ilhali zenyewe ndio wakiukaji wakubwa kabisa wa haki za binadamu na zinapaswa kuwajibishwa.

Kutokana na yote hayo tunaweza kusema kuwa, madai ya kutetea haki za binadamu yanayotolewa na Marekani na Ulaya ni mzaha mchungu wa kisiasa wa zama hizi, kwa sababu nchi hizo ni dhihirisho halisi la ukiukaji wa haki za binadamu duniani.../