Siku ya Haki za Binadamu za Kiislamu yaadhimishwa Tehran
Siku ya Haki za Binadamu za Kiislamu imeadhimishwa Jumanne mjini Tehran kwa kuwaleta pamoja wanaharakati za haki za binadamu.
Mwanaharakati wa haki za binadamu nchini Iran, Mohammad Vahedi amehutubu katika kikao hicho na kusema ubaguzi wa rangi nchini Marekani ni mfano wa wazi wa ukiukwaji wa haki za binadamu. Ameongeza kuwa ukandamizaji wa wananchi wanaoandamana Marekani kupinga ubaguzi wa rangi ni sehemu tu ya taswira halisi ya Marekani.
Vahedi ambaye ni mkurugenzi wa asasi isiyo ya kiserikali ya kutetea haki za binadamu inayojulikana kama Solh-e-Ziba (Amani Maridadi) amesema katika miongo ya hivi karibuni baadhi ya madola makubwa duniani yametumia vibaya kadhia ya haki za binadamu kwa maslahi yao.
Ameongeza kuwa, mabadiliko katika haki za binadamu yameathiri vibaya uhusiano baina ya nchi na kwa msingi huo ametoa wito wa kuwepo asasi zaidi za kutetea haki za binadamu.
Naye mwanaharakati wa kisiasa katika Jeshi la Kujitolea la Wananchi wa Iraq (PMU) Abdulkarim al-Haytham amehutubu katika kikao hicho na kusema, katika miongo ya hivi karibuni, nchi yake imeshuhudia ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na utumiaji wa mabomu yenye kemikali za sumu, mauaji ya kiholela, na kuwekwa watu vizuizini bila kufunguliwa mashtaka. Aidha ameongeza kuwa, uvamizi wa Marekani dhidi ya Iraq haujaleta chochote nchini humo isipokuwa uporaji na uharibifu.
Mwanadiplomasia wa zamani wa Iran nchini Misri Mojtaba Amani kwa upande wake amesema uwepo wa Marekani katika eneo ni chanzo cha ukosefu wa amani mbali na kuwa ni kizuizi katika kuimarika nguvu za mataifa ya Waislamu.
Shirika la Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) liliitangaza Agosti 5 kuwa Siku ya Haki za Binadamu za Kiislamu kufuatia pendekezo ambalo liliwasilishwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.