Majeshi ya Iran yako tayari kujenga hospitali mbili za muda Lebanon
-
Meja Jenerali Bagheri
Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, majeshi ya Iran yako tayari kujenga hospitali mbili za muda kwa ajili ya watu wa Lebanon iwapo serikali ya nchi hiyo itatoa ombi.
Meja Jenerali Bagheri, Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Jeshi la Iran na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) yako tayari kujenga hospitali mbili za muda nchini Lebanon zitakazokuwa na vifaa na madaktari kutoka Iran. Huku akitoa salamu za rambi rambii kwa watu na serikali ya Lebanon kufuatia kupoteza maisha Walebanon katika mlipuko wa Bandari ya Beirut, Meja Jenerali Bagheri amesema Majeshi ya Iran yako tayari kuisaidia Lebanon katika nyanja zote.
Aidha amesema Iran itatoa msaada wowote unaohitajika kwa Lebanon wakati wa kujenga upya bandari ya Beirut.
Tayari Hilali Nyekundu ya Iran imeshatuma shehena kubwa ya misaada kwa watu wa Lebanon sambamba na kujenga hospitali ya muda mjini Beirut kutoa huduma kwa waliojeruhiwa.
Moto uliozuka katika moja ya maghala ya bandari ya Beirut Jumanne, ulienea na kusababisha mlipuko mkubwa katika maghala mengine ya jirani kulikokuwa kumewekwa Ammonium nitrate. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Lebanon kufikia sasa kwa uchache watu 150 wamepoteza maisha na wengine zaidi ya 5000 kujeruhiwa katika mlipuko huo.