Kiongozi Muadhamu: Madola ya kikoloni yanayafanya mataifa yajihisi duni ili yaweze kuyadhibiti
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Madola ya kikoloni na ya kibeberu yanatumia kila njia kuyafanya yajihisi duni mataifa yanayotaka kuyahodhi na kuyatawala.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye mitandao ya kijamii kwa mnasaba wa kumbukumbu ya mwaka uliposainiwa mkataba wa udhalilishaji wa mwaka 1919 kati ya Uingereza na Iran.
Amesema: Mfano mmojawapo wa hilo ni mkataba wa 1919 uliosainiwa na Vossug ed Dowleh. Waliweza kufikia lengo lao nchini la kujenga hali ya udunishaji, ya kuwadhalilisha wananchi na kuonyesha kuwa taifa zima halina mamlaka yoyote na haliwezi kufanya chochote.

Tarehe 9 Agosti 1919, Waziri Mkuu wa wakati huo wa Iran Vossug ed Dowleh na Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati huo wa Uingereza Lord Curzon walisaini mkataba ambao ni mashuhuri kwa jina la Mkataba wa 1919 (Anglo-Persian Agreement).
Kwa mujibu wa mkataba huo, taasisi na vyombo vyote ya kijeshi na vya masuala ya fedha vya Iran viliwekwa chini ya usimamizi wa Waingereza na mamlaka ya uendeshaji njia ya reli ya Iran pia walipatiwa Waingereza.
Ilisemekana kuwa Vossug ed Dowleh na mawaziri wawili wa serikali yake walipokea hongo ya donge nono la fedha kutoka serikali ya Uingereza kwa ajili ya kufunga mkataba huo.../