Mousavi: Baadhi ya nchi za kinafiki zimejaribu kujionyesha kama watetezi wa Walebanon
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Abbas Mousavi amesema baadhi ya nchi zenye misimamo ya kinafiki zimejaribu kujionyesha kama watetezi wa watu wa Lebanon.
Mousavi ameyasema hayo mjini Tehran katika mkutano wa kila wiki na waandishi habari ambapo bila kuzitaja nchi hizo ameongeza kuwa, mlipuko uliojiri Jumanne katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut ulikuwa wa kusikitisha. Mousavi amesema baadhi ya nchi zimejaribu kuonyesha eti zinafungamana na watu wa Lebanon lakini kama kweli zina nia njema zinapaswa kuondoa vikwazo dhidi ya serikali na watu wa Lebanon.
Amesema uchunguzi kuhusu mlipuko huo ungali unaendelea na kwamba katika masaa ya awali kabisa ya tukio hilo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilisimama bega kwa bega na watu na serikali ya Lebanon. Amesema Rais Hassan Rouhani wa Iran aliamuru timu maalumu ya kutuma misaada Lebanon iundwe na hadi sasa ndege kadhaa za misaada zimeshafika mjini Beirut na misaada zaidi itaendelea kutumwa.
Kuhusiana na maandamana ambayo yameibuka Lebanon kufuatia mlipuko wa Beirut, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema mlipuko huo ulikuwa tukio kubwa na ni jambo linalotarajiwa kwa wananchi kuwa na hasira lakini jambo ambalo halikubaliki ni kwa baadhi ya watu, makundi au nchi za kigeni kutumia maandamano hayo kufikia malengo ya kisiasa. Amesema taifa la Lebanon limewahi kupita katika vipindi vigumu huko nyuma na hivyo serikali inapaswa kupewa fursa ya kuwashughulikia watu walioathiriwa na mlipuko huo.
Jumanne iliyopita mji mkuu wa Lebanon, Beirut ulikumbwa na mlipuko mkubwa ambao umeua zaidi ya watu 160 na kujeruhi wengine zaidi ya elfu sita. Mlipuko huo pia umesababisha hasara kubwa za kiuchumi zinazokadiriwa kufikia mabilioni ya dola.
Kampuni moja ya kutengeneza baruti ya Msumbiji imetangaza kuwa, shehena ya mzigo iliyokuwa imesimamishwa katika bandari ya Beirut ambayo ilisababisha mlipuko wa tarehe 4 Agosti ilikuwa mali ya kampuni hiyo.
Shehena hiyo ilikuwa na mada zinazotumiwa kutengeneza baruti kwa ajili ya mashirika ya kuchimba migodi nchini Msumbiji na ilikuwa ikishikiliwa katika bandari ya Beirut kwa karibu miaka saba.