Ali Rabiei: Iran itajibu hatua yoyote ya uchochezi ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i62739-ali_rabiei_iran_itajibu_hatua_yoyote_ya_uchochezi_ya_marekani
Msemaji wa Serikali ya Iran amekosoa muswada uliopendekezwa na Marekani kwa ajili ya kurefusha vikwazo vya silaha dhidi ya Iran na kusema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itajibu vikali hatua yoyote ya kichochezi ya Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 11, 2020 01:51 UTC
  • Ali Rabiei
    Ali Rabiei

Msemaji wa Serikali ya Iran amekosoa muswada uliopendekezwa na Marekani kwa ajili ya kurefusha vikwazo vya silaha dhidi ya Iran na kusema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itajibu vikali hatua yoyote ya kichochezi ya Marekani.

Ali Rabiei amesema kuwa njama haribifu za Marekani za kutaka kurefushwa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran zitabadilika na kuwa janga kubwa la kufeli na kutengwa zaidi serikali ya Washington. Ameongeza kuwa, msimamo wa Wamarekani wa kung'ang'ania njia iliyofeli hauna maana nyingine ghairi ya ukaidi na kukataa kukubali uhalisia wa mambo.

Rabiei ameongeza kuwa, ukweli ni kwamba jamii ya kimataifa imeazimia kulinda sheria, makubaliano na kanuni zinazotawala mahusiano ya nchi mbalimbalina na kusimama kidete mbele ya njama za Marekani za kutaka kuteteresha misingi ya amani ya kimataifa.

Msemaji wa Serikali ya Iran amesema kuwa, Marekani inataka kutumia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya taasisi za kimataifa na kuongeza kuwa: Hatua hiyo ya Washington inachezea shere na kukiuka taratibu za kimataifa na Baraza la Usalama lenyewe.

Muswada uliopendekezwa na Marekani kwa ajili ya kurefushwa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran unatazamiwa kuwasilishwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Jumatatu, na wanachama wa baraza hilo watakuwa na masaa 24 kutoa maoni yao kuhusu muswada huo. Russia na China ambazo ni wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama zimetangaza kuwa zinapinga muswada huo wa Marekani.

Azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama linasisitiza kuwa vikwazo vyote vya silaha dhidi ya Iran vinapaswa kuondolewa ifikapo tarehe 18 Oktoba mwaka 2020.