Mousavi: Marekani haijawahi kutengwa kiasi hiki
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa, haijawahi kushuhudiwa kuona Marekani ikitengwa kiasi hiki katika historia ya miaka 75 ya Umoja wa Mataifa. Sayyid Abbas Mousavi amebainisha hayo katika radiamali yake kwa kushindwa pakubwa Marekani mkabala na Iran katika Baraza la Usalama la UN.
Sayyid Abbas Mousavi ameandika leo katika ukurasa wake wa twitter kwamba, licha ya kufanyika ziara zote, mashinikizo na kuzunguka huku na kule Marekani imeshindwa hata kuishawishi nchi moja tu iiunge mkono.
Mousavi ameongeza kuwa, jana usiku diplomasia hai ya Iran pamoja na nguvu ya kisheria ya mapatano ya JCPOA kwa mara nyingine tena viliweza kuifelisha Marekani ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Azimio lililopendekezwa na Marekani kwa ajili ya kuongeza muda wa marufuku ya silaha dhidi ya Iran jana usiku lilishindwa kupasishwa baada ya Ubeljiji, Estonia, Ufaransa, Ujerumani, Indonesia, Niger, Saint Vicent, Afrika Kusini, Tunisia, Uingereza na Vietnam kujizuia kupiga kura, huku Marekani na Jamhuri ya Dominican zikipiga kura ya kuliunga mkono na Russia na China zikipiga kura ya hapana.