Kumbukumbu ya kurejea nchini Iran mateka wa Vita vya Kulazimishwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i62850-kumbukumbu_ya_kurejea_nchini_iran_mateka_wa_vita_vya_kulazimishwa
Tarehe 17 Agosti 1990 taifa la Iran lilishuhudia kuanza kurejea katika ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu mateka wa Vita vya Kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran walioachiliwa huru baada ya kutekwa na kufungwa kwa miaka mingi na utawala wa Kibaathi wa Iraq.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 16, 2020 21:56 UTC
  • Kumbukumbu ya kurejea nchini Iran mateka wa Vita vya Kulazimishwa

Tarehe 17 Agosti 1990 taifa la Iran lilishuhudia kuanza kurejea katika ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu mateka wa Vita vya Kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran walioachiliwa huru baada ya kutekwa na kufungwa kwa miaka mingi na utawala wa Kibaathi wa Iraq.

Mateka hao walioachiliwa huru walianza kurejea nchini ikiwa ni wiki mbili baada ya utawala huo huo wa Saddam Hussein wa Iraq kushambulia na kuiteka nchi nyingine jirani ya Kuwait. Siku mbili baada ya tukio hilo, Saddam alimwandikia barua Rais Hashimi Rafsanjani wa Iran akimjulisha uamuazi wa Iraq kutambua tena rasmi Mkataba wa Algiers uliotiwa saini mwaka 1975 na wakati huo huo kukubali masharti ya Iran ya kusimamisha vita.

Katika kipindi chote cha miaka minane ya Vita vya Kulazimishwa, taifa la Iran lilionyesha umoja, mshikamano, ukakamavu, ujasiri, hamasa na kujitolea kukubwa mbele ya adui mvamizi aliyekuwa akisaidiwa kwa hali na mali na karibu nchi zote za Magharibi na Kiarabu. Katika kipindi hicho umoja, mshikamano na fahari ya kitaifa iliwapa askari na mateka wa Iran moyo na ujasiri wa kuweza kusimama imara mbele ya adui bila ya kuogopa lolote.

Hii leo mwaka wa 41 wa Mapinduzi ya Kiislamu unapita katika hali ambayo moyo huo huo wa taifa hili kusimama kwa ushujaa na kujiamini mbele ya mabeberu wa dunia umeimarika hata zaidi.

Dikteta Saddam (kulia) aliyechochewa na Wamagharibi kuishambulia Iran

Ayatullah Ali Khamanei, Kiongozi Muashamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa taarifa akiashiria kipindi hicho cha kujitetea kutakatifu mbele ya maadui na kusema kuwa kilikuwa kipindi kilicholiletea taifa la Iran heshima kubwa. Amesisitiza kwa kusema: '.. Licha ya kuwa Vita vya Kulazimishwa vilililetea taifa la Iran hasara kubwa ya kimaada na kimaanawi lakini ni wazi kuwa katika kipindi hiki cha miaka minane ya kujitetea kutakatifu taifa la Iran lilipata faida nyingi zaidi kuliko hasara.....Uzoefu wa miaka minane ya kujitetea kutakatifu umethibitisha wazi kwamba licha ya kuwepo vizingiti, mashinikizo, uhaba wa fedha na matatizo mengi, inawezekana kukabiliana na mataifa yanayotumia mabavu na yenye tamaa duniani...Ni mapambano hayo ya kishujaa ya taifa la Iran yaliyoonyeshwa katika miaka minane ya Vita vya Kujitetea Kutakatifu ndiyo yaliyowashajiisha watu wengine wenye nyoyo na fikra safi katika nchi za Kiislamu na zisizo za Kiislamu kusimama imara dhidi ya maadui huku wakiwa mikono mitupu kwa ajili ya kutetea imani zao.....'

Kwa mtazamo huo kipindi cha Vita vya Kulazimishwa ni akiba yenye thamani kubwa kwa ajili ya kupambana na kuwashinda maadui. Ni kutokana na ukweli huo ndipo hamasa kubwa na ya kujivunia ya kipindi cha Vita vya Kujitetea Kutakatifu pamoja na subira na uvumilivu mkubwa ulioonyeshwa na wafungwa wa vita utaendelea kubakia milele kama ukurasa wenye fahari kubwa wa mapambano ya kishujaa ya taifa kubwa la Iran mbele ya maadui.

Uzoefu wa kipindi hicho unathibitisha wazi kwamba sharti la kufikiwa uhuru na kujitawala, utukufu na heshima ni mapambano yanoyofungamana na subira na uvumilivu kwa sababu ni mapambano na uvumilifu mbele ya matatizo tu ndio unaweza kumdhaminia mwanadamu ushindi wa mwisho.

Kundi la kwanza la mateka wa vita kurejea nchini Iran

Hii leo athari na matokeo ya mapambano mbele ya adui yanaoonekana wazi katika nyanja tofauti za mapambano. Ni wazi kuwa ubunifu na vipawa vya watu hudhihiri na kustawi wakati wa shida na matatizo. Kwa kutilia maanani ukweli huo, tunaweza kusema kuwa mapambano katika medani za vita na subira na uvumilivu katika kipindi kigumu cha kukamatwa mateka ni masuala mawili muhimu yaliyodhamini ushindi wa kipindi cha vita na kujitetea kutakatifu.

Masoud Rezai, mwandishi na mtafiti anasema ushindi wa taifa la Iran unatokana na moyo wa mapambano na kuongeza kuwa: Uzoefu wa mapambano umewathibitishia watu wa Iran kwamba subira na uvumilivu mbele ya matatizo, jitahada katika njia ya Mwenyezi Mungu na matumaini ya ushindi mkabala na maadui ni suala muhimu katika kufikiwa malengo ya Mapinduzi na ya umma.

Kwa mtazamo huo, kumbukumbu ya kurejea nchini kwa ushindi metaka wa Vita vya Kulazimishwa, kunakumbushia hamasa ambayo si tu kuwa ni yenye thamani kubwa kwa kizazi cha leo bali kwa vizazi vingine vyote vitakavyokuja baadaye.