Wanafunzi nusu milioni raia wa kigeni wanasoma Iran bila malipo
Waziri wa Elimu Nchini Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatoa elimu bila malipo yoyote kwa zaidi ya wanafunzi nusu milioni wa kigeni.
Mohsen Haji Mirzai, Waziri wa Elimu nchini Iran ameyasema hayo leo katika mahojiano na IRNA alipoulizwa kuhusu wanafunzi wa kigeni wanaosoma Iran. Ameongeza kuwa wanafunzi wa kigeni wanasoma na wenzao wa kigeni na wanapata huduma zote ambazo wanafunzi Wairani wanapata.
Haji Mirzai aidha ameashiria kuhusu masomo ya wanafunzi wa kigeni nchini Iran katika kipindi hiki cha janga la corona na kusema: "Masomo ya raia wa kigeni na Wairani hayatafautiani kwa sababu sera za Iran ni sawa kwa wanafunzi wote wawe wa kigeni au Wairani."
Waziri wa Elimu pia ametoa wito kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi na taasisi zote husika za kimataifa kutekeleza majukumu yao kuhusu wanafunzi wa kigeni ambao ni wakimbizi nchini Iran.
Kwa mujibu wa Idara ya Raia wa Kigeni katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran, karibu watu milioni moja na nusu wamejisajili rasmi nchini Iran na kuna wakimbizi wengine milioni mbili ambao hawana vibali au vitambulisho. Aghalabu ya wakimbizi hao ni kutoka nchi jirani ya Afghanistan.
Katika fremu ya sisitizo la mara kwa mara la Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, wahajiri Waafghani wanaoishi nchini Iran wawe wako nchini kisheria au kinyume cha sheria, wanapaswa kupata masomo bila malipo na pia wapate huduma zote za kiafya na matibabu bila kubaguliwa.
Wakuu wa Umoja wa Mataifa wameishukuru Iran mara kadhaa kwa kuwapokea kwa ukarimu wakimbizi kutoka Afghanistan.