Zaidi ya wagonjwa 304,000 wa Covid-19 nchini Iran wamepata afueni
Msemaji wa Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu ya Iran amesema, wagonjwa wengine wapya zaidi ya elfu mbili wa maradhi ya Covid-19 wamegunduliwa nchini, huku idadi ya waliopata afueni ya ugonjwa huo ikipindukia 304,000.
Sima Sadat Lari, msemaji wa Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu ya Iran ameyaeleza hayo leo wakati akitoa takwimu mpya za watu waliokumbwa na virusi vya corona hapa nchini Iran na akabainisha kuwa: Kwa mujibu wa matokeo ya vipimo rasmi, katika muda wa saa 24 zilizopita wagonjwa wapya 2,279 waliokumbwa na ugonjwa wa Covid-19 wamegunduliwa hapa nchini, ambapo 1,038 miongoni mwao wamelazwa hospitali na waliosalia wamepatiwa huduma za tiba na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Bi Lari amefafanua kuwa, idadi ya watu waliougua ugonjwa wa Covid-19 nchini Iran imefikia 352,558 na kutokana na wagonjwa 139 kuaga dunia katika kipindi cha saa 24 zilizopita, jumla ya watu waliofariki kutokana na ugonjwa huo hadi sasa imefikia 20,264.
Kadhalika msemaji wa Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu ya Iran amesema kuwa, hadi kufikia leo mchana, wagonjwa 304,236 wamepata afueni na kuruhusiwa kutoka hospitalini na kurejea majumbani.
Wakati huo huo, idadi ya watu walioambukizwa virusi vya corona duniani imepindukia milioni 22 huku kwa akali laki 7 na 90,000 kati yao wakiwa wameaga dunia.
Marekani imeendelea kuwa nchi ya kwanza duniani kwa kuathiriwa vibaya zaidi na maambukizo ya virusi vya Corona ikifuatiwa na Brazil, India na Russia.