Uwezo mkubwa wa Iran katika uzalishaji wa silaha za kistratijia
Iran kuwekewa vikwazo vya silaha kwa muda mrefu huenda kukawafanya baadhi ya watu kudhani kwamba baada ya kuondolewa vikwazo hivyo Iran ilipasa kubadilika na kuwa soko kubwa la mauzo ya silaha kwa maslahi ya nchi zinazozalisha silaha duniani ama ukweli wa mambo ni kinyume kabisa na dhana hii.
Akizungumza hapo siku ya Jumanne na wanachama wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Kigeni ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) mara tu baada ya kutembelea maonyesho ya bidhaa na zana za ulinzi za Wizara ya Ulinzi ya Iran, Brigedia Jenerali Amir Hatami, Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisisitiza katika kikao na wanachama wa kamisheni hiyo kwamba, Wizara ya Ulinzi ya Iran inaendelea vyema na juhudi zake za kuimarisha usalama wa kitaifa na kulinda nguvu ya kuzuia hujuma na mashambulizi ya adui.
Ameashiria uwezo na miundomsingi ya Wizara ya Ulinzi katika kudhamini mahitaji ya kiulinzi ya nchi na kusema: Wizara ya Ulinzi iko tayari kutumia uwezo wake wa kielimu katika uwanja wa ulinzi kusaidia sekta za uchumi na zisizo za kijeshi za nchi na hasa katika mwaka huu uliokusudiwa kuongeza maradufu uzalishaji wa taifa.
Ikiwa ni katika juhudi zake za kujilinda na licha ya kuwepo vizingiti na vikwazo ambavyo vimekuwa vikitekelezwa tokea wakati wa vita vya kulazimishwa vya miaka minane na hata baada ya kipindi hicho, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imethibitisha kivitendo kwamba imeweza kutumia uwezo wa ndani ya nchi kupiga hatua kubwa kimaendeleo.
Utengenezaji wa makombora ni moja ya sekta ambazo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilihisi kwamba inahitajia kujiimarisha baada ya kumalizika kipindi cha vita na leo kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu, imeweza kupiga hatua kubwa katika kutengeneza makombora ya kisasa yakiwemo ya cruise na ya balistiki, na hivyo kuwa miongoni mwa nchi chache duniani zinazotenegeneza makombora ya aina hiyo. Maendeleo hayo makubwa yamepelekea wataalamu wengi wa masuala ya kijeshi na kisiasa ulimwenguni kuamini kuwa leo kumedhihiri uwiano mpya wa kijeshi na masuala ya usalama kwa manufaa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Antonio Cartolucci Mchambuzi wa Kimarekani wa masuala ya jiopolitiki alisema mara tu baada ya kurushwa angani kwa mafanikio satalaiti ya kijeshi ya Iran inayoitwa Nour: Iran ni moja ya nchi muhimu za dunia ambazo zinachangia pakubwa katika uwepo wa kambi kadhaa zenye nguvu duniani.
Katika uwanja wa ulinzi wa baharini pia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepiga hatua kubwa katika uwanja huo. Kuundwa nchini kwa nyambizi za Ghadir na Fateh ambazo kila moja ina sifa zake maalumu ni mojawapo ya maendeleo makubwa yaliyofikiwa katika uwanja huo. Sekta ya utengenezaji wa ndege zisizo na rubani, au droni, ni suala jingine ambalo limeifanya Iran kuwa nguvu ya kwanza katika eneo zima la Asia Magharibi, na ya nne duniani katika uwanja huo.
Iran vilevile imepiga hatua kubwa ya kiulinzi katika sekta ya makombora ya kutungua ndege na vyombo vingine vya angani. Mifumo ya makombora ya Bovar 373, Khordad 3, Kamin 2, Tabas na Sayad ni mifumo muhimu ya ulinzi wa anga ambayo imetengenezwa na wataalamu wa humu humu nchini, ambapo kila mmoja una nafasi yake maalumu na madhubuti katika ngome ya ulinzi wa anga ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Katika sekta ya mifumo ya ulinzi wa leza ambapo ni nchi chache mno duniani ambazo zina uwezo wa kuwa na nafsi katika sekta hiyo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kuingia na kuwa na nafasi muhimu katika sekta hiyo.
Kuimarika katika sekta ya ulinzi kwa hakika kunahesabiwa kuwa nguzo muhimu na ya kistratijia katika uwanja wa ulinzi na hasa inapotiliwa maanani kuwa uwezo huo wa kiulinzi unatokana na elimu na teknolojia ya wataalamu wa humu humu nchini. Ni kwa kutilia maani mwenendo na uwezo huo mkubwa wa kiulinzi wa Iran ndipo waziri wa ulinzi wa taifa hili akasisitiza kuwa, Iran haina tatizo lolote katika uzalishaji wa zana za kijeshi za kisasa na za kistartijia.