Maulamaa wa Kisunni Iran walaani makubaliano ya Israel na UAE
Wanazuoni wa Kisunni hapa nchini Iran wamekosoa vikali mapatano yaliyofikiwa hivi karibuni kati ya Umoja wa Falme za Kiarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya pande mbili hizo.
Katika taarifa, Maulamaa wa Kisunni nchini Iran wamesema makubaliano hayo ya fedheha baina ya Israel na Imarati yamewavunja moyo Waislamu kote duniani.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa, kutokana na kitendo hicho cha kifidhuli, Umoja wa Falme za Kiarabu sasa unatambulika kama Umoja wa Falme za Kiyahudi katika fikra za wapigania haki kote duniani.
Wanazuoni wa Kisunni hapa nchini Iran wameeleza katika taarifa hiyo kuwa, makubaliano ya namna hii ya aibu baina ya Marekani, utawala haramu wa Israel na baadhi ya tawala vibaraka za Kiarabu yametoa pigo si tu kwa Waislamu na ulimwengu wa Kiislamu, bali pia kwa utu na ubinadamu.
Wamesisitiza kuwa, kuwatetea Wapalestina madhulumu na Quds Tukufu kunasalia kuwa kadhia kuu katika Umma wa Kiislamu na ni fedheha isiyo na mfano kwa baadhi ya tawala za Kiarabu kujidhalilisha na kujiuza kama bidhaa kwa maadui wa Uislamu na Mtume wa Uislamu (SAW).
Agosti 13, pande mbili za Abu Dhabi na Tel Aviv zilisaini mkataba na kuafikiana rasmi kuanzisha uhusiano kamili wa kidiplomasia, chini ya kile kilichotajwa kama upatanishi wa Marekani.
Makubaliano hayo kati ya Israel na Imarati yamekabiliwa na wimbi kali la malalamiko na upinzani wa makundi ya Palestina, nchi za Kiislamu katika eneo la Asia Magharibi na shakhsia kadhaa wa kisiasa, kijamii na kidini kote duniani.