Ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiulinzi baina ya Iran na Russia kufunguliwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i63023-ukurasa_mpya_wa_ushirikiano_wa_kiulinzi_baina_ya_iran_na_russia_kufunguliwa
Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, baada ya kumalizika vikwazo vya silaha dhidi ya Iran, kutafunguliwa ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiulinzi baina ya Tehran na Mascow.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 25, 2020 07:23 UTC
  • Ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiulinzi baina ya Iran na Russia kufunguliwa

Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, baada ya kumalizika vikwazo vya silaha dhidi ya Iran, kutafunguliwa ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiulinzi baina ya Tehran na Mascow.

Brigedia Jenerali Amir Hatami amesema hayo katika mahojiano yaliyorushwa hewani leo Jumanne na televisheni ya "Russia 24" na kuongeza kuwa, muda wa mwisho wa kuweko vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran ni tarehe 17 Oktoba mwaka huu na kwamba Iran na Russia zitakuwa na ushirikiano mkubwa zaidi wa kiulinzi kupitia mikataba mbalimbali zitakayowekeana baada ya vikwazo hivyo.

Amesema, vikwazo vimewafanya vijana wa Iran waigeuze nchi hii kuwa mzalishaji wa silaha na kupata mafanikio makubwa katika uwanja huo. Ameongeza kuwa Tehran na Moscow hazina njia nyingine isipokuwa kushirikiana katika kukabiliana na mashinikizo na siasa za kibeberu za Marekani.

Mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Russia katika picha ya pamoja

 

Waziri wa Ulinzi wa Iran aidha amesema, vikosi vya ulinzi vya Iran vinapaswa kuimarishwa kwa namna ambayo adui atambue kwamba iwapo atafanya uchokozi wowote basi atapata hasara na maafa makubwa maradufu ya yale atakayoisababishia Iran.

Brigedia Jenerali Amir Hatami pia amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe haitoruhusu magaidi wafanye uharibifu kama walioufanya katika nchi za Iraq na Syria na kusisitiza kuwa, magenge ya kigaidi ni tishio si kwa Iran, Iraq na Syria tu, bali ni hatari kubwa pia kwa Russia.

Waziri wa Ulinzi wa Iran amefanya ziara ya siku mbili nchini Russia kwa mwaliko wa waziri mwenzake Sergej Sjojgoe (Sergey Shoygu) ambapo katika ziara hiyo mbali na kuonana na viongozi mbalimbali wa nchi hiyo, alitembelea pia maonyesho ya kimataifa ya kijeshi ya Russia yanayojulikana kwa jina la ARMY20.,