Iran yaendelea kuboresha sekta yake ya ulinzi baada ya vita vya
-
Nembo ya Wizara ya Ulinzi ya Iran
Wizara ya Ulinzi ya Iran imesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu inaendelea kuifanya sekta yake ya ulinzi kuwa ya kisasa, ikizingatia mahitaji yaliyojitokeza kutokana na vita vya hivi karibuni vilivyolazimishwa dhidi ya nchi hii na Marekani na Israel.
Katika taarifa iliyotolewa Alhamisi wizara imesema: “Vita hivi vya karibuni vilivyolazimishwa vilitupa fursa ya kupata uelewa sahihi zaidi wa uwezo wetu, kubaini mahitaji mapya na kuweka mwelekeo wa siku zijazo. Tumejifunza kwamba hatupaswi kamwe kusimama.”
“Kwa msingi huo, tunaichukulia vita vya hivi karibuni vya kulazimishwa kuwa ni vita vya zamani; bila kujivunia kupita kiasi wala kuwa na hofu, tunaendelea kujiboresha, kuibuni upya na kuisasisha sekta ya ulinzi kwa kuzingatia matokeo na mafunzo haya.”
Wizara hiyo imebainisha kuwa uwezo wa ulinzi wa Iran, uliotengenezwa kwa miaka mingi na wataalamu wa Iran, pamoja na uwezo wa kiutendaji wa Majeshi ya Iran na msimamo thabiti wa taifa la Iran, “ulivuruga sehemu kubwa ya hesabu na malengo ya adui na kuwaacha katika mshangao.”
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, vita vya hivi karibuni pia vilionyesha kuwa umoja ndio “msingi” wa usalama wa kitaifa, unaowezesha kuendelea kwa nguvu na maendeleo ya nchi.
Taarifa hiyo ilitolewa kabla ya Siku ya Kitaifa ya Sekta ya Ulinzi, inayoadhimishwa tarehe 31 ya mwezi wa Mordad katika kalenda ya Kiirani; tarehe hiyo itaangukia Agosti 22 mwaka huu.
Taarifa hiyo imesema: “Mordad 31 ni siku ya kukumbuka kwa fahari njia ambayo taifa la Iran limeipitia katika kujenga uwezo wake wa ulinzi na viwanda; njia iliyoanza katika miaka migumu na yenye matukio mengi, na iliyochipuka kutokana na uzoefu wa kihistoria wa mapambano ya kupata uhuru na kujinasua kutoka katika minyororo ya ukoloni na utegemezi, vikwazo na vitisho.”
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa vikwazo na vitisho vimeongeza azma ya nchi ya kutegemea uwezo wake wa ndani. Aidha Wizara ya Ulinzi ya Iran imekumbusha kuwa: “Njia hii iliandaliwa, ikasanifiwa na kuhandisiwa chini ya uongozi na mwongozo wa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.”
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, dhamira ya wazi ya wizara ni “kubadilisha uzoefu wa uwanja wa vita kuwa maarifa, maarifa kuwa teknolojia, na teknolojia kuwa uwezo wa ulinzi wa siku zijazo.”
“Njia hii itaendelea kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu, chini ya uongozi wa kimkakati wa Mheshimiwa Ayatullah Sayyid Mojtaba Hosseini Khamenei, na kwa uungaji mkono wa wananchi wa Iran pamoja na juhudi za kizazi kipya cha wanasayansi, wataalamu na vijana wa nchi hii.”