Iran: Huwi tena gaidi ukishamlipa pesa Trump
Mkurugenzi Mkuu wa Asia Magharibi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amesema kuhusu pendekezo lililotolewa na Marekani kwa Sudan la kuitaka ilipe dola milioni 330 ili jina la nchi hiyo liondolewe kwenye orodha ya ugaidi ya Washington kwamba: Huwi tena gaidi ukishamlipa pesa Trump.
Sayyid Rasoul Mousavi, ambaye ni msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje na Mkurugenzi Mkuu wa Asia Magharibi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kuhusiana na safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo nchini Sudan kwamba: Katika serikali iliyo chini ya urais wa Donald Trump kitu chochote kile kinaweza kuuzwa au kununuliwa.
Marekani imeipendekezea Sudan ilipe dola milioni 330 kwa raia wa Marekani walioathirika kutokana na mashambulio ya mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda, ili jina la Khartoum liondolewe kwenye orodha ya Washington ya nchi zinazofadhili ugaidi.

Pendekezo hilo lililotolewa hivi karibuni na Washington kwa Sudan la kulipa pesa ili jina la nchi hiyo liondolewe kwenye orodha ya waungaji mkono wa ugaidi limeamsha hasira za wananchi katika mji mkuu Khartoum.
Katika safari aliyofanya siku ya Jumanne nchini Sudan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo alitangaza pia uungaji mkono wa Washington kwa serikali ya mpito ya nchi hiyo.../