Iran: Siasa za kujikumbizia kila kitu upande wake Marekani zaidhoofisha UN
Mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa usiku wa kuamkia leo ameandika kwenye ukurasa wa kijamii wa Twitter kwamba, siasa za Marekani za kujikumbizia kila kitu upande wake zinaudhoofisha Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la umoja huo.
Majid Takht-Ravanchi amesema hayo kujibu madai ya viongozi wa Marekani yanayohusiana na kurejea vyenyewe kwa vyenyewe vikwazo dhidi ya Iran na kuongeza kuwa, dharau za Marekani kwa sheria za kimataifa zimevunja tena rekodi. Amesema, Washington si tu imevunja makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lakini pia inafanya makusudi kutoa tafsiri ghalati na isiyo sahihi ya azimio hilo na wakati huo huo inatoa vitisho hata kwa waitifaki wake wa karibu mno kutokana na kutokubaliana kwao na siasa hizo za kibeberu za Marekani.
Juzi Alkhamisi, Mike Pompeo, waziri wa mambo ya nje wa Marekani aliandika katika Twitter kwamba licha ya Baraza la Usalama kupinga azimio la White House dhidi ya Iran lakini vikwazo vya Umoja wa Mataifa vitarejea vyenyewe kwa vyenyewe usiku wa manane wa tarehe 20 Septemba kwa wakati wa Greenwich.
Katika ukurasa wake huo wa Twitter, Pompeo amedai kuwa, Marekani imeanzisha mchakato wa "Snapback Mechanism" wa kurejesha vikwazo vyote vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran baada ya kufeli juhudi zake katika Baraza la Usalama la umoja huo.
Ametoa madai hayo licha ya kwamba si mwanachama tena wa mapatano ya nyuklia ya JCPOA baada ya kujitoa kijeuri kwenye makubaliano hayo. Vile vile ametoa vitisho kwa mwanachama yeyote wa Baraza la Usalama atakayepinga hatua yake hiyo.