Umbumbumbu wa Marekani katika masuala ya sheria, wameshindwa na sasa wanatoa vitisho
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amekosoa jitihada zinazofanywa na Marekani kwa ajili ya kurejesha vikwazo vya kimataifa dhidi ya Iran kuanzia tarehe 20 Oktoba mwaka huu wa 2020 na kusema: Viongozi wa serikali ya Marekani ni mbumbumbu katika masuala ya sheria na hawajui lolote kuhusiana na tendaji wa Umoja wa Mataifa.
Muhammad Javad Zarif alisema jana katika ujumbe wake kwenye mtandao wa Twitter kwamba: Baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulikataa mara tatu ombi la Marekani sasa nchi hiyo inatishia kwamba itamuwekea vikwazo mtu au taasisi yoyote itakayozuia kurejeshwa vikwazo dhidi ya Iran.
Dakta Zarif ameiambia Marekani kwamba "muliitaliki JCPOA mwaka 2018. Jina lenu katika cheti cha ndoa halina maana tena."
Licha ya Baraza la Usalama la UN kupinga muswada wa kurefusha vikwazo vya silaha dhidi ya Iran lakini Alkhamisi iliyopita Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo, alisema kuwa, vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran vitahuishwa tena tarehe 20 Septemba.
Msimamo huo wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani umebainishwa baada muswada uliokuwa dhidi ya Iran wa Marekani kwa ajili ya kurefusha vikwazo vya silaha kushindwa katika Baraza la Usalama kutokana na uwezo wa kisiasa wa Jamhuri ya Kiislamu na udiplomsia makini wa Iran katika mashauriano yake na wanachama wa baraza hilo. Vilevile wanachama 13 wa Baraza la Usalama akiwemo Rais wa taasisi hiyo muhimu ya Umoja wa Mataifa, wamesisitiza kuwa, Marekani haina haki ya kisheria ya kutumia azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama kwa sababu si mwanachama tena katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Katika mkondo huo huo mwakilishi wa kudumu wa Russia katika jumuiya za kimataifa mjini Vienna, Mikhail Ulyanov, alisema jana kuhusu jitihada za Marekani katika Baraza la Usalama za kutaka kurejesha vikwazo dhidi ya Iran kwamba: Msimamo huu wa Marekani ni wa kifidhuli, na pendekezo la Washington na kutaka kutumiwa kipengee cha "Snapback Mechanism" kuhusu kadhia ya Iran halina mwelekeo wala mashiko ya kisheria.
Baada ya kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Marekani ilipoteza haki za kisiasa na kisheria za kuweza kutumia azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama kwa ajili ya kutekeleza siasa zake za mabavu dhidi ya Iran, na matunda pekee ya hatua hiyo ya Washington ni kuchekwa na kuchezewa shere Baraza la Usalama. Vilevile tunaweza kusema kuwa, hatua ya wanachama karibu wote wa Baraza la Usalama kuipa mgongo Marekani tena mara tatu katika suala la kurejeshwa vikwazo dhidi ya Iran inadhihirisha kilele cha kutengwa na kukataliwa siasa za serikali ya Washington katika medani ya kimataifa. Kwa sababu hiyo Seneta Chris Murphy wa chama cha Democratic anaamini kuwa: Kufeli muswada wa Marekai wa kutaka kurefusha vikwazo vya silaha dhidi ya Iran ni kipigo kibaya kwa nchi hii katika medani ya kimataifa.
Baada ya kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA hapo mwaka 2018, Marekani si mwanachama tena katika mapatano hayo na hivyo haina haki ya kutumia azimio 2231 la Baraza la usalama kwa sababu JCPOA ni sehemu ya azimio hilo ambalo Washington ililikanyaga na kulikiuka.
Kwa utaratibu huo msimamo wa Marekani wa kung'an'ania suala la kutumia azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama kwa ajili ya kutekeleza kipengee cha "Snapback Mechanism" na kurejesha vikwazo vya silaha vya kimataifa dhidi ya Iran ni kielelezo cha siasa haribifu za serikali ya Washington na sera za mabavu za White House ambazo yumkini zikateteresha nafasi ya kisheria na mustakbali wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.