Rais Rouhani: Mitazamo ya Iran na Niger katika masuala ya kimataifa inafanana
(last modified Tue, 01 Sep 2020 07:48:31 GMT )
Sep 01, 2020 07:48 UTC
  • Rais Rouhani: Mitazamo ya Iran na Niger katika masuala ya kimataifa inafanana

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika mazungumzo yake ya simu na mwenzake wa Niger kuwa nchi mbili hizi zimekuwa na ushirikiano amilifu na mitazamo inayofanana katika masuala na taasisi za kimataifa na kubainisha kuwa, nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika bila shaka itakabiliana na uchukuaji wa maamuzi ya upande mmoja wa Marekani katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Katika mazungumzo hayo ya simu na Rais  Mahamadou Issoufou wa Niger, Rais Rouhani ameeleza bayana kuwa, "nina uhakika kwamba Niger kama taifa huru na mwanachama wa Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM), itazuia kutumiwa vibaya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Marekani inayopenda kuchukua uamuzi wa upande mmoja; kama ilivyokataa kuburuzwa kupasisha azimio haramu la kurefushwa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran."

Dakta Rouhani amesema nchi mbili hizi zina mtazamo mmoja; kwamba mahusiano ya kimataifa yanapaswa kuwa katika misingi ya haki, uhuru, mshikamano, heshima, na thamani za utu. 

Kadhalika ameipongeza nchi hiyo ya Kiafrika na Kiislamu kwa kuendelea kuunga mkono makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na Azimio Nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusisitiza kwamba: Chimbuko la matatizo mengi duniani ni kutumiwa vibaya baadhi ya nchi katika taasisi za kimataifa.

Maafisa wa serikali ya Niger walipoitembelea Iran miaka micheche nyuma

Huku akishiria kuhusu miongo minne ya uhusiano wa kidugu na kirafiki na Niger, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema nchi mbili hizi zimekuwa na ushirikiano mzuri katika nyuga za uchimbaji madini, afya na kilimo na kwamba anatumai kuwa Tehran na Niamey zitatumia nguvu zao zote kupanua uhusiano huo.

Kwa upande wake, Rais Mahamadou Issoufou wa Niger amesema uhusiano wa pande mbili wa nchi yake na Iran umekuwa mzuri na wa kirafiki katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, hususan katika uga wa kukabiliana na janga la corona na kwamba nchi hiyo ya Afrika Magharibi ipo tayari kuimarisha zaidi uhusiano wa pande mbili. 

 

Tags