'Kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW, ni sura mpya ya ujinga wa kisasa'
Kamati ya Haki za Binadamu ya Chombo cha Mahakama cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza kuwa, kitendo kiovu cha jarida la Charlie Hebdo cha kuchapisha vibonzo vinavyomvunjia heshima Mtume Muhammad SAW ni sura mpya ya ujinga wa kisasa.
Charlie Hebdo ni jarida la vichekesho linalomilikiwa na watu wenye chuki na dini hasa ya Kiislamu nchini Ufaransa. Katika miaka ya 2012 na 2015 lilichapisha vibonzo vinavyomvunjia heshima Mtume Muhammad SAW na kusababisha maandamano makubwa katika nchi zote za Waislamu kulaani utovu huo wa adabu wa jarida hilo.
Kamati ya Haki za Binadamu ya Chombo cha Mahakama cha Iran imesema katika taarifa iliyotolewa jana kwamba kitendo cha jarida hilo la Ufaransa ndiyo hayo yanayodaiwa maendelea ambayo kimsingi hayajali heshima wala matukufu yoyote ya wanadamu, yanachezea shere utu, yameiteka na yanafanyia istihzai zawadi ya uhuru aliyopewa mwanadamu na Mola wake na yanawalazimisha wanadamu kuamini kwamba mambo ya kipuuzi eti ndio uhuru wa kweli.
Taarifa ya kamati hiyo imeongeza kuwa, kitendo kiovu cha kupotosha maana ya uhuru na kufanya ubaguzi katika mambo yanayohusiana na uhuru ni hatari kubwa kwa uhuru wa kweli katika dunia ya leo.
Aidha imeelezea kusikitishwa kwake na kushindwa vyombo na viongozi husika wa Ufaransa kulichukulia hatua jarida hilo na imewataka wanadamu wote wenye fikra huru duniani pamoja na mashirika yanayodai kutetea haki za binadamu yachukue hatua za kweli za kulinda maana sahihi na tukufu ya neno uhuru na yalaani uhalifu uliofanywa na jarida hilo la Ufaransa.