Mazishi ya Wapalestina 50 wasiojulikana waliouawa katika mauaji ya kimbari
Mamia ya watu wameswali Swala ya Janaza wakati wa mazishi ya pamoja katika Jiji la Gaza kwa ajili ya Wapalestina 50 ambao miili yao ilipatikana hivi karibuni na vikosi vya Ulinzi wa Raia ikiwa chini ya mabaki ya nyumba zilizobomolewa katika mashambulizi ya Israel wakati wa vita vya mauaji ya kimbari katika eneo hilo lililozingirwa.
Siku ya Alhamisi, Wapalestina walikusanyika katika viwanja vya Jengo la Afya la al-Shifa katika Jiji la Gaza kushiriki katika hafla ya kuwaaga na maziko yao katika makaburi ya jiji hilo.
Vikosi vya Ulinzi wa Raia vya Gaza viliweza kuipata miili ya Wapalestina hao zaidi ya miaka miwili baada ya kuuawa kwao.
Mamlaka ya Ulinzi wa Raia ya Gaza imewataka waandishi wa habari wa ndani na kimataifa, pamoja na taasisi za habari, kuhudhuria shughuli za mazishi ili kurekodi ukatili wa Israel na kuufikishia ulimwengu mzima mateso ya familia za Wapalestina waliopoteza wapendwa wao kutokana na mashambulizi ya Israel yaliyolenga nyumba na maeneo ya makazi.
Inadokezwa kuwa yamkini mashahidi hao walitoka katika familia za al-Sawafiri, al-Batniji na Karam. Walizikwa wakiwa hai baada ya dari za nyumba zao kuanguka kutokana na mashambulizi ya Israel.
Wizara ya Afya ya Gaza ilisema Alhamisi kwamba Wapalestina wengine 10 wameuawa na 25 wamejeruhiwa katika muda wa saa 24 zilizopita katika Ukanda wa Gaza, na hivyo kuongeza idadi ya waliofariki kutokana na mauaji ya kimbari ya Israel tangu Oktoba 2023 kufika 73,417.
Mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na Israel huko Gaza yamesababisha uharibifu mkubwa katika eneo lote la ukanda huo mwembamba wa pwani, huku takribani asilimia 90 ya miundombinu yake ikiathirika. Umoja wa Mataifa unakadiria gharama za ujenzi upya kufikia karibu dola bilioni 70. Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ICC, imetoa waranti wa kukamatwa waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na waziri wake wa zamani wa vita Yoav Gallant kutokana na jinai zao huko Gaza.