Mwelekeo mwema wa uhusiano wa Iran na wakala wa IAEA
Uhusiano wa Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) katika muda wa mwaka mmoja na nusu uliopita yaani katika kipindi cha uongozi wa Mkurgenzi Mkuu Rafael Grossi ulikuwa wa mwelekeo mbaya kutokana na wakala huo kuathiriwa na mashinikizo ya kisiasa na kutoa baadhi ya madai yasiyo na ushahidi wala uthibitisho kuhusiana na masuala ya huko nyuma.
Mtazamo huo hasi, hata hivyo, umebadilika baada ya safari iliyofanywa karibuni na Mkurugenzi wa IAEA mjini Tehran na mapatano yaliyofikiwa katika mazungumzo ya kiufundi kati ya Iran na wakala huo. Taarifa ya Tehran na baadaye taarifa ya Vienna ni kielelezo cha kufunguliwa ukurasa mpya katika uhusiano wa Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA).
Mkurugenzi Mkuu wa IAEA juzi Ijumaa alitoa ripoti akipongeza mapatano yaliyofikiwa kati ya Tehran na wakala huo. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki tarehe 26 mwezi Agosti mwaka huu zilitoa taarifa ya pamoja mwishoni mwa safari ya siku mbili ya Mkurugenzi Mkuu wa IAEA hapa Tehran. Taarifa hiyo ilieleza kuwa: Iran, kwa hiari yake, imeruhusu kukaguliwa maeneo mawili yaliyoainishwa na wakala wa IAEA na itafanikisha kazi ya uhakiki wa wakala huo kwa ajili ya kulipatia ufumbuzi suala hilo.
Kazem Gharibabadi Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Taasisi za Kimataifa huko Vienna pia amesema katika mahojiano na waandishi wa habari kuwa: Ripoti ya Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kuhusu makubaliano ya wakala huo na Jamhuri ya Kiislamu inashiria mustakbali mwema katika uhusiano wa pande hizo mbili.
Taarifa ya Tehran inaonyesha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina tatizo na wakala wa IAEA katika suala la kushirikiana na kukaguliwa baadhi ya maeneo. Kuhusu suala hilo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Muhammad Javad Zarif ameandika katika ukurasa wake wa twitter kwamba: "Iran haina kitu cha kuficha" na hii ndiyo njia ya utatuzi yaani kufikiwa mwafaka baina ya Tehran na wakala wa IAEA. Iwapo kutafikiwa mwafaka, basi kambi dhidi ya Iran ambayo Marekani inafanya jitihada za kuidumisha, itakuwa imefungwa."
Katika kuchambua suala hilo kuna mambo mawili yanayokaribiana sana kuhusu malengo ya Marekani dhidi ya Iran. Kwanza ni kutaka kuzusha mivutano kati ya Iran na IAEA na hili ndilo chaguo linalopewa kipaumbele zaidi na viongozi wa serikali ya Trump na baadhi ya wanasiasa wenye misimamo mikali katika Kongresi ya Marekani.
Pili ni kutakka kuimarisha mchakato wa kuitenga Iran kimataifa; jambo ambalo lingali miongoni mwa machaguo yaliyo mezani ya Marekani. Hata hivyo Marekani haikupata mafanikio katika njama hii. Baada ya kushindwa vibaya mara mbili ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yaani baada ya kukumbana na upinzani mkali katika jitihada zake za kutaka kurefusha vikwazo vya silaha dhidi ya Iran na kushindwa kutumia utaratibu wa Snapback Mechanism, sasa Marekani imeshindwa tena katika mkakati wake wa kuharibu uhusiano wa Iran na IAEA.
Marekani ilitaka kuitumia vibaya kadhia ya ukaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kuhusu Iran ili kuyadhoopfisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kuhalalisha siasa zake za mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi.
Kelsey Davenport Mkurugenzi wa Masuala ya Sera za Kuzuia Silaha za Nyuklia wa Taasisi ya Kudhibiti Silaha ya Washington anaamini kuwa: Mwenendo wa Iran wa kuheshimu mapatano ya nyuklia ya JCPOA umesaidia jitihada za nchi mbalimbali za kukabiliana na mashinikizo ya Marekani ya kutekelezwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran.