Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa kulaani kuvunjiwa heshima Bwana Mtume SAW
Dhambi kubwa na isiyosameheka ya gazeti moja la Ufaransa ya kumvunjia heshima Bwana Mtume SAW, kwa mara nyingine tena imedhihirisha chuki, adawa na ushari wa vyombo vya kisiasa na kiutamaduni vya Ulimwengu wa Magharibi dhidi ya Uislamu na jamii ya Waislamu.
Jumanne ya wikii iliyopita, jarida la Charlie Hebdo la Ufaransa kwa mara nyingine tena lilichukua hatua ya kifidhuli ya kuchapisha katuni na vibonzo vinavyomvunjia heshima Mtume Muhammad (S.A.W). Katika ujumbe wake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu sambamba na kuashiria nukta kadhaa muhimu kuhusiana na suala hilo amelaani vikali kuvunjiwa heshima Mtume wa Uislamu Muhammad al-Mustafa SAW. Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema kuwa, kisingizio cha 'uhuru wa kujieleza' kinachotumiwa na wanasiasa wa Ufaransa ili wasilaani jinai hiyo ni kosa kubwa na upotoshaji wenye maslahi ya kisiasa na kueleza kwamba, sera za Wazayuni na madola ya kiistikbari zilizo dhidi ya Uislamu ndilo chimbuko la vitendo hivi vya kiuhasama.
Harakati za makundi potovu na haribifu katika vyombo vya habari vya Magharibi sambamba na miamala michafu ya baadhi ya makundi mabaya na potovu ambayo kila baada ya muda fulani hudhihirisha vitendo vyao vya kishenzi kwa kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu na thamani nyingine za kidini, yanafuatilia malengo tofauti ambayo hayana uhusiano wowote na taasubi za kidini wala za kimadhehebu na ni hatua ambazo hata haiwezekani kuzitetea na kuzihalalisha kwa msingi na mtazamo wa uhuru wa kutoa maoni au itikadi.
Harakati hizi ambazo zimepitwa na wakati, kabla ya hapo zilikwishang'amuliwa na watu wenye umaizi na utambuzi wa dini na thamani za kidini na hata fikra za waliowengu ulimwenguni zinatambua kwamba, chochokochoko hizi ni zao la vituo vya kifikra vya Uzayuni na Uistikbari. Duru hizo zinafuatilia suala la kuzipotosha fikra za walio wengi ulimwenguni kuhusiana hali mbaya na taabani ya utamaduni wa Magharibi mkabala wa matatizo ya kiutamaduni, kijamii na fedheha za viongozi wa kibeberu mbele ya malalamiko makubwa yanayowakabili katika nchi hizo. Hata hivyo, hatupaswi kughafilika na jambo hili kwamba, kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu ni njama ambayo daima iliandaliwa mipango hapo kabla na yenye malengo maalumu.
Tukitupia jicho faili la huko nyuma kuanzia mchoraji wa vikatuni wa Denmark hadi kwa kasisi aliyeivunjia heshima Qur'ani Tukufu inafahamika vyema kwamba, harakati na mipango hii imeratibiwa tangu kale.
Nyuma ya pazia ya harakati hiyo potovu kuna harakati muhimu ya kisiasa kwa anuani ya lengo la kistratejia ambayo hatupaswi kughafilika nayo. Katika nukta hii hatupaswi kutilia shaka kwamba, kuna malengo ya siri na ya nyuma ya pazia ya hatua hizi za kuvunjia heshima matukufu ya Kiislamu nayo ni kuzipotosha fikra za Waislamu kuhusiana na kadhia ya Palestina ambayo inahesabiwa kuwa kadhia muhimu na inayopewa kipaumbele katika Ulimwengu wa Kiislamu.
Hasa kwa kutilia maanani kwamba, hivi sasa kadhia ya Palestina inaandamwa na mipango michafu na ya kisherani kama Muamala wa Karne na kuanzisha uhusiano wa kawaida na adui khabithi wa ubinadamu yaani utawala bandia wa Israel.
Ni kwa kutilia mkazo nukta hii ambapo, katika ujumbe wake wa kulaani kuvunjiwa heshima Mtume SAW, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akaeleza kwamba: Kutekelezwa kitendo hiki wakati huu kunaweza kukawa na msukumo wa kupotosha fikra na akili za wananchi na tawala za Kiarabu katika eneo la Asia Magharibi kuhusiana na mipango michafu ambayo Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel zinayo kwa ajili ya eneo hili. Waislamu hususan wa mataifa ya Asia Magharibi sambamba na kuwa macho kuhusiana na masuala nyeti ya eneo hili, hawapaswi katu kusahau uadui wa wanasiasa na viongozi wa Magharibi dhidi ya Uislamu na Waislamu.
Kulinda uhuru wa kujieleza au uhuru wa maoni kumetumiwa kama kisingizio cha kutokabiliana na matusi na hatua hizi za kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu, lakini upande mwingine wa kadhia ambao unapaswa kuzingatiwa ni kwamba, hili limegeuzwa na kuwa mchezo mchungu wa kuigiza wa kisiasa katika zama hizi.
Katika hali ambayo, kitendo hiki haiwezekani hata kidogo kukitolea hoja na maneno ya kukitetea, Rais wa Ufaransa ambaye nchi yake kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa inashuhudia malalamiko ya kila Jumamosi anathubutu kuhusisha kitendo cha kuvunjiwa heshima Mtume SAW na Qur'ani Tukufu na uhuru wa kutoa maoni; lakini katika jamii hiyo hiyo ya Ulaya ambayo kama wanavyodai viongozi wake inaamini suala la uhuru wa kujieleza na kutoa maoni au hata uhuru wa itikadi, kukosoa na kukana ngano ya Holocaust adhabu yake ni kifungo jela.
Hapana shaka kuwa, vitendo kama hivi havina hatima nyingine ghairi ya kufedheheka zaidi misimamo na miamala ya kindumakuwili ya wale wanaodai kuwa ni vinara wa kutetea uhuru wa kutoa maoni na haki za binadamu.