Wanasheria nchini Iran walaani kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad SAW
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i63316-wanasheria_nchini_iran_walaani_kuvunjiwa_heshima_mtume_muhammad_saw
Wanasheria hapa nchini Iran wamelaani vikali hatua ya jarida la Kifaransa la Charlie Hebdo ya kumvunjia heshima Bwana Mtume SAW.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 09, 2020 03:37 UTC
  • Wanasheria nchini Iran walaani kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad SAW

Wanasheria hapa nchini Iran wamelaani vikali hatua ya jarida la Kifaransa la Charlie Hebdo ya kumvunjia heshima Bwana Mtume SAW.

Wanasheria wapatao 5,000 hapa Iran jana walitoa taarifa rasmi ambapo sambamba na kukemea vikali kitendo hicho cha kishenzi wameeleza kwamba, hilo ni dhihirisho jingine la demokrasia ya kiliberali na ujinga mamboleo.

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imeeleza kwamba, hatua chafu ya gazeti la Kifaransa la Charlie Hebdo ni mfano wa wazi wa uenezaji chuki na uvunjiaji heshima matukufu ya Kislamu na kukiuka wazi haki ya uhuru wa kidini.

Aidha wanasheria hao wamesema, kitendo hicho kinakiuka bayana kipengee nambari 1 na 18 cha tangazo la Haki za Binadamu kama ambavyo kwa mujibu wa kipengee cha 32 cha sheria ya uhuru wa magazeti  nchini Ufaransa kitendo hicho ni kosa na uhalifu.


"Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote"- Qur'ani 21:107

 

Jumatano iliyopita, kwa mara nyingine tena jarida la Kifaransa la Charlie Hebdo liliamua kwa makusudi kuwafanyia kejeli na istihzai Waislamu na dini tukufu ya Uislamu kwa kuchapisha vibonzo vinavyomvunjia heshima Mtume Muhammad SAW.

Hivi karibuni, watu wenye chuki dhidi ya Uislamu walichoma moto na kuteketeza nakala ya Qur'ani katika mji wa Malmo nchini Sweden.  Vitendo hivyo vya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu vimeendelea kulaaniwa na wapenda haki, watu huru na wenye dhamira safi kote ulimwenguni hususan katika Ulimwengu wa Kiislamu.