Sababu za vita vya kulazimishwa na umuhimu wa kujitetea kutakatifu
Utawala wa Baath wa Iraq tarehe 21 Septemba mwaka 1980 ulivamia ardhi ya Iran na kuanzisha vita dhidi ya Jamhuri iliyokuwa changa ya Kiislamu hapa nchini. Vita hivyo vilivyoendelea kwa kipind cha miaka 8 vilianzishwa kwa mujibu wa mpango maalumu na kwa baraka na amri ya Marekani kwa ajili ya kuiondoa madarakani Jamhuri ya Kiislamu.
Katika kipindi chote cha miaka 8 ya vita hivyo maadui walimuunga mkono na kumsaidia kwa hali na mali Saddam Hussein na majeshi yake dhidi ya Iran lakini hawakuweza kutimiza malengo yao. Katika mtazamo huo kipindi cha miaka 8 ya vita vya kujitetea kutakatifu kina nukta na thamani zitakazoendelea kuwepo siku zote ambazo hii leo ni nguzo muhimu na imara ya taifa la Iran mbele ya njama na uhasama wa maadui zake.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema jana alihutubia sherehe ya kuwaenzi wakongwe wa vita vya kujitetea kutakatifu vilivyoanzishwa na Saddam Hussein dhidi ya Iran kupitia njia ya video na kusema kuwa: Katika vita hivyo taifa la Iran lilisimama kidete mbele ya madola ya Mashariki na Magharibi na nchi tegemezi, na kuibuka na ushindi. Alifafanua umuhimu wa mapambano na muqawama wa taifa la Iran katika kipindi cha vita vya kujitetea kutakatifu na kusema ulikuwa na nafasi na mchango muhimu katika kubadili mlingano wa kivita na katika kuzima njama kubwa iliyokuwa imepangwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, kujitetea kutakatifu katika kipindi hicho nyeti kumewekeza sana kwa ajili ya nchi na kuibua rasilimali kubwa ya yenye thamani. Katika kipindi hicho kulijitokeza hamasa kubwa kama kukombolewa mji wa Khorramshahr na ushindi mwingine mkubwa. Wakati huo Marekani na nchi za Ulaya zilizokuwa sikimsaidia Saddam katika vita dhidi ya Iran, zilitayarisha mazingira ya kuendelea vita hivyo kwa kuupa utawala wa Baathi aina mbalimbali za silaha ili kwa madai yao, awezi kuungusha utawala wa Kiislamu nchini Iran.
Hapana shaka kuwa miongoni mwa matunda muhimu ya kipindi cha vita vya kujitetea kutakatifu ni kuimarisha amani hapa nchini. Kujitetea kutakatifu kumeonyesha kuwa, mashambulizi na uvamizi dhidi ya Iran yana gharama kubwa kwa wavamizi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa wapiganaji wa makundi ya kujitolea ya Walinzi wa Haram ni mfano wa baraka za kipindi cha vita vya kujitetea kutakatifu na kuendelea kwa moyo wa kupigana jihadi ndani ya kizazi kipya. Ameongeza kuwa: Kuwepo kwa wapiganaji wa mataifa mbalimbali ya Iran, Syria, Iraq, Lebanon na Afghanistan katika safu moja ya Walinzi wa Haram ni miongoni mwa matukio ya kustaajabisha ya zama hizi.
Ukweli ni kwamba, kipindi cha vita vya kujitetea kutakatifu ambacho kimejaa thamani nyingi, sasa kimekuwa sehemu ya utambulisho wa kitaifa wa Iran. Suala hilo liliashiriwa katika hotuba ya jana ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye ametilia mkazo udharura wa kuwa macho mbele ya njama za adui za kutaka kupotosha ukweli kuhusu kipindi cha vita vya kujitetea kutakatifu.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, Saddam Hussein mpenda jaha alikuwa wenzo wa madola makubwa hususan Marekani na kuongeza kuwa: Upande asili wa vita hivyo dhidi ya taifa la Iran, yaani Marekani iliyopata kichapo kutokana na ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, madola yaliyokuwa na wasiwasi kutokana na kujitokeza utambulisho mpya wa Kiislamu na Kiirani katika eneo la Magharibi mwa Asia, NATO na nchi za Ulaya Mashariki na Magharibi, zilimhamasisha Saddam kuishambulia Iran ili kutokomeza kabisa utawala na Mapinduzi ya Kiislamu. Ameongeza kuwa: Katika vita hivyo taifa la Iran lilisimama kidete mbele ya madola ya Mashariki na Magharibi na nchi tegemezi, na kuibuka na ushindi.
Kipindi cha vita vya miaka 8 ya kujitetea kutakatifu ni hazina yenye thamani kubwa kwa taifa la Iran kinachoakisi uwezo mkubwa ya taifa mbele ya maadui na hivyo hapana budi kulinda matunda yake, kuyaenzi na kuyabakisha hai siku zote.