Ayatullah Ibrahim Raisi: Nchini Marekani polisi inachukiwa sana
Mkuu wa Vyombo vya Mahakama vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kubainisha kuwa, nchini Marekani kikosi cha polisi kinachukiwa mno amesema, kukandamiza shingo kwa goti dhidi ya waandamanaji na kubinya sauti zao si uthibitisho wa kuwa na nguvu na uwezo.
Ayatullah Ibrahim Raisi amesema hayo leo hapa mjini Tehran kwa mnasaba wa kuanza Wiki ya Kikosi cha Polisi nchini Iran na kusisitiza kwamba, kuna tofauti baina ya kuwa na nguvu na kutumia mabavu.
Mkuu wa Vyombo vya Mahakama vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya raia wanaopigania uadilifu vinavyoshuhudiwa hii leo nchini Marekani na barani Ulaya na kukandamiza shingo zao kwa kutumia magoti kwa lengo la kuzima sauti zao katu si ishara ya kuwa na nguvu na uwezo jeshi la polisi.
Ayatullah Raisi amebainisha kwamba, kuwaunga mkono wananchi na kuwalinda ni miongoni mwa vigezo na sifa muhimu za kikosi cha polisi.
Mkuu wa Vyombo vya Mahakama vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekemea na kulaani vikali ukandamizaji unaofanywa na vyombo vya usalama nchini Marekani.
Itakumbukwa kuwa, George Floyd aliyekuwa na umri miaka 46 aliaga dunia baada ya kukandamizwa shingoni kwa goti na polisi mzungu kwa jina la Derek Chauvin kwa muda wa dakika tisa huko Minneapolis jimboni Minnesota Mei 25 mwaka huu.
Kifo cha kikatili cha raia huyo Mmarekani mweusi mwenye asili ya Afrika kiliibua maandamano makubwa nchini Marekani na katika nchi nyingine huku watu wakiendelea kupinga vitendo vya mabavu vya polisi na ubaguzi wa rangi nchini Marekani.