Chanjo ya COVID-19 iliyotengenezwa Iran kuanza kufanyiwa majaribio wanadamu
Chanjo ya COVID-19 iliyotengenezwa nchini Iran itaanza kufanyiwa majaribio kwa wanaadamu mapema mwezi ujao wa Novemba.
Akizungumza na waandishi habari Jumanne, Waziri wa Afya wa Iran Daktari Saeed Namaki amesema kuna makundi matano ambayo yanajishughulisha na uundwaji wa chanjo hiyo na kwamba makundi mawili yameweza kupata matokeo mazuri. Amesema Iran imebuni njia muafaka za kukabiliana na virusi vya COVID-19 na tayari imeshalifahamisha Shirika la Afya Duniani, WHO kuhusu hatua ilizopiga.
Amesema kuna matumaini makubwa kuwa katika mustakabali wa karibu, watu wa Iran watapata habari njema kuhusu chanjo ya COVID-19 iliyoundwa humu nchini.
Waziri Namaki amesema iwapo watu wote watazingatia kanuni za kukabiliana na COVID-19, kasi ya kuenea ugonjwa huo itapungua.
Huku hayo yakijiri Msemaji wa Wizara ya Afya ya Iran Bi Sima-Sadat Lari jana Jumanne alisema kumeripotiwa kesi 5,039 za COVID-19 nchini Iran na kufanya idadi ya walioambukizwa kufika 539,670. Ameongeza kuwa wagonjwa 434, 676 wamepona na wengine 4,810 wamelazwa hospitalini wakiwa mahututi. Aidha amesema katika kipindi cha masaa 24 hadi kufikia jana adhuhuri, watu 322 walikuwa wamepoteza maisha kutokana na corona na kufanya idadi ya walipoteza maisha kuwa 31,034. Hadi sasa watu zaidi ya milioni nne na nusu wamepimwa COVID-19 kote Iran.