Watu 415 wafariki dunia kwa corona nchini Iran
Msemaji wa Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu ya Iran ametangaza habari ya kugunduliwa zaidi ya wagonjwa 6,000 wapya wa ugonjwa wa COVID-19 humu nchini na kufarikia dunia wagonjwa 415 katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita.
Daktari Sima Sadat Lari, amesema hayo leo Jumatano wakati akitoa takwimu mpya za watu waliokumbwa na kirusi cha corona hapa Iran na kuongeza kuwa: Kwa mujibu wa matokeo ya vipimo rasmi, katika muda wa masaa 24 yaliyopita wagonjwa wapya 6,824 waliokumbwa na ugonjwa wa COVID-19 wamegunduliwa humu nchini, ambapo 2,490 miongoni mwao wamelazwa hospitalini na waliosalia wamepatiwa huduma za tiba na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Msemaji wa Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu ya Iran ameongeza kuwa, idadi ya watu waliogunduliwa kupatwa na ugonjwa wa COVID-19 nchini Iran hadi hivi sasa imefikia 558,648 na kutokana na wagonjwa 415 kuaga dunia katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita, jumla ya watu waliofariki dunia hapa nchini kutokana na ugonjwa huo hadi sasa imefikia 31,714.
Aidha afisa huyo wa Wizara ya Afya ya Iran amesema kuwa, kufikia leo mchana, wagonjwa 467,917 wameshapata afueni na kuruhusiwa kutoka hospitalini na kurejea majumbani.
Katika upande mwingine hadi kufikia leo mchana, idadi ya watu waliokumbwa na kirusi cha corona duniani kote imepindukia milioni 44 na laki 3 na 54 elfu. Miongoni mwa hao, watu zaidi ya 1,173,782 wameshaaga dunia na wengine zaidi ya 32,503,603 wamepata nafuu na kuruhusiwa kutoka hospitalini.
Marekani imeendelea kuwa nchi iliyoathiriwa zaidi na kirusi cha corona duniani baada ya zaidi ya watu milioni 9 na 39,170 kuambukizwa kirusi hicho, ikifuatiwa na India, Brazil, Russia, Ufaransa, Uhispania, Argentina, Colombia na UIngereza. Zaidi ya wagonjwa 232,101 wa corona wameshafariki dunia nchini Marekani pekee.