Zarif: Amani haiwezi kupatikana kwa kuchochea mataifa mengine
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i64318-zarif_amani_haiwezi_kupatikana_kwa_kuchochea_mataifa_mengine
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, amani haiwezi kupatikana kupitia njia ya kuyachochea mataifa na wafuasi wa dini nyingine.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 30, 2020 03:10 UTC
  • Muhammad Javad Zarif
    Muhammad Javad Zarif

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, amani haiwezi kupatikana kupitia njia ya kuyachochea mataifa na wafuasi wa dini nyingine.

Muhammad Javad Zarif ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalaani vikali shambulizi la kigaidi lililotokea katika mji wa Nice nchini Ufaransa na kuongeza kuwa: Nafasi ya mzunguko huu batili wa kuzidisha uhasama, kueneza chuki, uchochezi na ukatili inapaswa kuchukuliwa na mantiki na utumiaji wa akili na busara. 

Dakta Zarif amesema pande zote zinapaswa kuelewa kuwa, uchupaji mipaka unafuatiwa na uchupaji mipaka zaidi, na haiwezekani kupatikana amani kwa vitendo au matamshi ya kichochezi. 

Rais Macron wa Ufaransa analaumiwa kwa kutoa matamshi ya kichochezi dhidi ya Waislamu

Watu wasiopungua watatu waliuawa jana na wengine kadhaa walijeruhiwa waliposhambuliwa na mtu aliyekuwa na kisu ndani ya kanisa la Notre Dame lililopo katika mji wa Nice. 

Hayo yanajiri huku uhusiano wa Ufaransa na Ulimwengu wa Kiislamu ukiwa umeingia doa baada ya matamshi ya kichochezi yaliyotolewa na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron akitetea vitendo vya kumtusi na kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW ndani ya nchi hiyo.