Nchi za Kiislamu ziunde komandi ya pamoja ya kutatua matatizo ya Waislamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i64342-nchi_za_kiislamu_ziunde_komandi_ya_pamoja_ya_kutatua_matatizo_ya_waislamu
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu ametilia mkazo udharura wa kuundwa komandi kuu ya pamoja ya nchi za Kiislamu kwa ajili ya kutatua matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 31, 2020 04:08 UTC
  • Nchi za Kiislamu ziunde komandi ya pamoja ya kutatua matatizo ya Waislamu

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu ametilia mkazo udharura wa kuundwa komandi kuu ya pamoja ya nchi za Kiislamu kwa ajili ya kutatua matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu.

Hujjatul Islam Hamid Shahriyari amesema hayo katika mkutano wa 34 wa kimataifa wa Wiki ya Umoja wa Kiislamu unaofanyika kwa njia ya Intaneti na kuongeza kuwa, kuna wajibu kwa Waislamu kushirikiana zaidi na zaidi katika kutatua migogoro iliyopo hivi sasa katika ulimwengu wa Kiislamu. Amesema, kuundwa jopo kazi la pamoja la kutatua migogoro hiyo na kuuongoza ulimwengu wa Kiislamu katika njia sahihi, ni jambo la dharura sana hivi sasa.

Kwa upande wake, Sheikh Waqar Ahmad, mjumbe wa Jumuiya ya Kiislamu ya jimbo la Rajasthan nchini India amesema katika mkutano huo uliofanyika jana usiku kwamba kuna wajibu kwa Waislamu kuwasaidia watu wote wanaokumbwa na matatizo duniani kwani kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu, kuwasaidia watu wengine ni ibada.

 

Amesema, kuwasaidia watu wengine ni sehemu muhimu ya mafundisho ya Uislamu na kusisitiza kuwa, hivi sasa ambapo walimwengu wanateseka kwa ugonjwa wa COVID-19, Waislamu wako mstari wa mbele kuwasaidia watu wengi ili kwa pamoja iwezekane kuiokoa dunia na janga hili. Amesema hayo ndiyo maadili bora yaliyofundishwa na Mtume Muhammad SAW.

Mkutano wa 34 wa kimataifa wa Umoja wa Kiislamu ulianza juzi Alkhamisi tarehe 29 Oktoba 2020 kwa njia ya Intaneti na utaendelea hadi keshokutwa Jumatatu. Zaidi ya wasomi na wanachuoni 160 wakubwa wa ulimwengu wa Kiislamu kutoka nchi 47 duniani wanashiriki katika mkutano huo. Washiriki wanaunganishwa kwa njia ya video kutokea nchini Iran.