Zarif: Iran haistahamili uwepo wa magaidi karibu na mipaka yake
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ametahadharisha kuhusu suala la kuhamishiwa na kuwepo makundi ya kigaidi katika mgogoro wa Nagorno-Karabakh.
Muhammad Javad Zarif ambaye mapema leo alikuwa akizungumza na televisheni ya taifa ya Iran kuhusiana na machafuko na ukosefu wa amani unaosababishwa na kuhamishiwa magaidi hususan mabaki ya kundi la Daesh katika eneo la Karabakh na mashauriano ya jinsi ya kukabiliana na magaidi hao, amesema kuwa Iran inajua vyema kwamba, magaidi wanashiriki katika vita vya eneo hilo na kwamba Tehran inasisitiza kuwa suala hilo halitakuwa na maslahi kwa upande wowote.
Zarif amesema katika mazungumzo ya karibuni, Iran iliwajulisha maafisa wa Jamhuri ya Azerbaijan, Armenia, Russia na Uturuki suala la kupelekwa na kuwepo makundi ya kigaidi katika eneo la Karabakh na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu haitastahamili jambo hilo.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameashiria mpango uliopendekezwa na Jamhuri ya Kiislamu kwa ajili ya amani ya eneo la Nagorno-Karabakh na kusema: Mpango huo wa amani wa Iran hauhusiani na suala la kusitishwa vita kwa muda bali unajumuisha masuala mengi ikiwa ni pamoja na kundoka majeshi vamizi katika maeno yote yaliyovamiwa.
Jamhuri ya Azerbaijan na Armenia zinahitilafiana kuhusu eneo la Nagorno-Karabakh katika mzozo ulianza mwaka 1988. Vita vya sasa baina ya nchi hizo mbili vilianza tarehe 27 Septemba na hadi sasa majeshi na raia wa kawaida wa pande hizo mbili wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa.