Wanazuoni na wahubiri wa Kiislamu wa Iran walaani kutusiwa Mtume Muhammad SAW
Wanazuoni na wahubiri wa Kiislamu wa Vyuo Vikuu vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zaidi ya elfu mbili wamelaani vikali kitendo cha kutusiwa na kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad SAW nchini Ufaransa.
Katika taarifa yao, wanazuoni na wahubiri wa Kiislamu wa Vyuo Vikuu vya Iran wapatao 2,400 wamesema taifa la kibeberu ambalo kwa miaka mingi katika enzi za ukoloni liliwatesa na kuwakandamiza watu wa nchi lilizozikoloni barani Afrika, na kupora rasilimali zao walizopewa na Mwenyezi Mungu, hii leo kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza, linaruhusu kuvunjiwa heshima matukufu ya kidini na thamani za utu.
Huku wakilaani kitendo hicho cha kihaini cha Ufaransa cha kuruhusu kuchapishwa vibonzo vya kumtusi Mtume Muhammad SAW, wanazuoni na wahubiri hao wa Kiislamu wa Vyuo Vikuu vya Iran wamesema Uislamu ni dini ya utu na hadhi, na Mtume wa Uislamu SAW ni rehema kwa walimwengu wote, na ka msingi huo kumtusi ni sawa na kuzitusi dini nyinginezo na Mitume wengineo.
Katika hatua nyingine, Jumuiya ya Kiislamu ya Ufilipino imemuandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ikimtaka atoe taarifa ya kulaani kitendo cha Ufaransa cha kumtusi Mtume Mtukufu Muhammad SAW.
Katika barua hiyo, jumuiya hiyo imesema inasikitisha kuona vitendo vya kuumiza nyoyo Waislamu bilioni moja na nusu duniani vimefanyika nchini Ufaransa, tena kwa uungaji mkono wa rais wa nchi.
Sehemu moja ya barua hiyo imesema: Kwa kuwa kazi kubwa ya Umoja wa Mataifa ni kudumisha amani duniani, tungependa kukufahamisha kuwa Uislamu ni dini ya amani na urafiki, na Mtume Muhammad ni mbeba bendera wa haki na amani. Bwana Macron halitizami suala la kutilia shaka na kukashifu eti mauaji ya Mayahudi ya Holocaust kama mfano wa uhuru wa kujieleza, lakini anashajiisha kutusiwa Mtume Mtukufu SAW.
Jumuiya ya Kiislamu ya Ufilipino imesema katika hali ambayo haiungi mkono vitendo vya kihaini na kufurutu ada, inataraji kuwa Katibu Mkuu wa UN atafanya juhudi za makusudi za kuwaunga mkono Waislamu, na kuzuia kutukanwa matukufu ya dini hiyo.