"Serikali ijayo ya Marekani haina budi kusalimu amri mbele ya Iran"
Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema serikali ijayo ya Marekani haitakuwa na chaguo jingine ghairi ya kusalimu amri mkabala wa Jamhuri ya Kiislamu.
Rais Rouhani amesema hayo mapema leo katika uzinduzi wa mradi wa kusambaza maji kutoka Ghuba ya Uajemi hadi mikoa ya Iran ya Kerman na Yazd na kukariri kuwa, Tehran haijali ni nani atakayeibuka mshindi katika uchaguzi wa rais wa Marekani uliofanyika juzi Jumanne.
Amesema, "si muhimu kwetu sisi ni mgombea yupi ataibuka mshindi. Jambo la uhakika ni kuwa, serikali ijayo (ya Marekani) bila shaka itajisalimisha kwa taifa la Iran."
Dakta Rouhani amesisitiza kuwa, serikali ya Washington haina budi kuheshimu sheria, kanuni na mashinikizo ya fikra za walio wengi, na vile vile kusalimu amri mkabala wa subira na muqawama wa taifa la Iran.
Rais wa Iran amebainisha kuwa, katika kipindi cha miezi minane iliyopita, taifa hili limefanikiwa pakubwa kudhibiti msambao wa virusi vya corona, licha ya vikwazo, mashinikizo, changamoto na matatizo mbalimbali.
Ameeleza bayana kuwa, mashinikizo hayawezi kulipigisha magoti taifa kubwa la Iran, na kwamba kutokana na kusimama kidete taifa hili, maadui watalazimika kurejea katika mkondo wa kuheshimu sheria.