Kamanda: Iran haitaruhusu anga yake iwe sehemu ya kufanyia majaribio
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i64538-kamanda_iran_haitaruhusu_anga_yake_iwe_sehemu_ya_kufanyia_majaribio
Kamanda wa Kikosi cha Ulinzi wa Anga cha Khatamul Anbia cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezionya pande hasimu katika mgogoro wa Armenia na Jamhuri ya Azerbaijan dhidi ya kufanya kosa la kuhujumu anga ya nchi hii.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 10, 2020 03:58 UTC
  • Kamanda: Iran haitaruhusu anga yake iwe sehemu ya kufanyia majaribio

Kamanda wa Kikosi cha Ulinzi wa Anga cha Khatamul Anbia cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezionya pande hasimu katika mgogoro wa Armenia na Jamhuri ya Azerbaijan dhidi ya kufanya kosa la kuhujumu anga ya nchi hii.

Brigedia Jenerali Qader Rahimzadeh alitoa onyo hilo jana Jumatatu na kusisitiza kuwa: Anga ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran si sehemu ya kufanyia majaribio ya pata potea.

Ameeleza bayana kuwa, Vikosi vya Ulinzi vya Iran vipo macho na tayari kabisa kukabiliana na yeyote anayehujumu anga yake. Brigedia Jenerali Qader Rahimzadeh amesema Tehran haiwezi kunyamazia kimya kosa la kuhujumiwa anga yake.

Haya yanajiri siku chache baada ya Jeshi la Nchi Kavu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutuma zana za kivita na wanajeshi katika mpaka wa nchi hii na Armenia na Azerbaijan. Maeneo ya mpakani katika mkoa wa Azerbaijan mashariki mwa Iran yanapakana na Jamhuri ya Azerbaijan na Armenia, nchi mbili ambazo zimekuwa zikipigania eneo linalozozaniwa la Nagorno Karabakh.

Mapigano katika eneo linalozozaniwa la Nagorno Karabakh

Tokea mgogoro wa Nagorno Karabakh uanze hadi sasa mamia ya maroketi ya pande mbili hasimu yamekuwa yakidondoka katika eneo la Khoda Afarin ambalo lina mpaka wa kilomita 135 na nchi mbili zinazozozana.

Haya yanajiri katika hali ambayo, Armenia na Azerbaijan kwa upatanisho wa Russia, zimesaini makubaliano ya kusitisha vita kikamilifu na kuondoa wanajeshi wao katika eneo la Nagorno Karabakh.