Watu 546,000 wamepona corona Iran hadi sasa
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Afya ya Iran Daktari Sima Sadat Lari ametangaza leo kuwa, hadi sasa watu 738,000 wameambukizwa corona au COVID-19 nchini na kuwa miognoni mwao 546,642 wamepona.
Aidha amesema katika kipindi cha masaa 24 hadi kufikia adhuhuri ya leo, watu 461 wamepoteza maisha kutokana na corona na kupelekea idadi kamili ya vifo hadi sasa kuwa 40,582. Hali kadhalika amesema wagonjwa 5,630 wa corona wako katika hali mahututi.
Daktari Sadat Lari amesema nchini Iran hadi sasa watu 5,424,479 wamepimwa corona.
Huku hayo yakijiri Naibu Waziri wa Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu wa Iran anayehusika na teknolojia na utafiti amesema, chanjo ya ugonjwa wa COVID-19 iliyobuniwa hapa nchini iko kwenye awamu ya utengenezaji.
Reza Malikzadeh ameyasema hayo leo na kusisitiza kuwa, watafiti na wataalamu wa Iran wanafanya juhudi kwa uwezo wao wote ili kuhakikisha utengenezaji na uzalishaji wa chanjo hiyo unafanikishwa.
Malikzadeh ameeleza kwamba, mwanzoni mwa mripuko wa maambukizi ya corona ilidhaniwa kuwa chanjo ya ugonjwa wa COVID-19 itakuwa na uwezo wa kutoa kinga kwa asilimia 50, lakini utengenezaji wa chanjo mpya umeonyesha kuwa chanjo hiyo itakuwa na uwezo wa kutoa kinga kwa zaidi ya asilimia 90.