Chanjo 5 za COVID-19 za Iran zinasubiri kupasishwa na WHO
Msemaji wa Shirika la Chakula na Madawa la Iran ametangaza kuwa, chanjo 5 za corona zilizotengenezwa nchini Iran, hivi sasa zinasubiri kupasishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Shirika la habari la IRNA limemnukuu Daktari Kianush Jahanpur akiandika hayo jana Ijumaa katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa, hadi kufikia sasa kuna chanjo tano za Iran kwenye orodha ya chanjo za COVID-19 zinazosubiri kupasishwa na WHO.
Jitihada za kuzalisha chanjo za ugonjwa hatari wa corona zinafanywa na nchi mbalimbali duniani ambapo hivi karibuni baadhi ya mashirika ya kuzalisha madawa yametangaza habari ya kufanikiwa kwa asilimia 90 katika juhudi hizo.
Kabla ya hapo pia, Naibu Waziri wa Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu wa Iran anayehusika na teknolojia na utafiti alikuwa amesema kwamba, chanjo ya ugonjwa wa Covid-19 iliyobuniwa humu nchini iko kwenye awamu ya utengenezaji.
Reza Malikzadeh alisema hayo mapema jana Ijumaa na kusisitiza kuwa, watafiti na wataalamu wa Iran wanafanya juhudi kwa uwezo wao wote kuhakikisha utengenezaji na uzalishaji wa chanjo hiyo unafanikishwa kwa njia bora kabisa.
Ameeleza kwamba, mwanzoni mwa mripuko wa maambukizi ya corona ilidhaniwa kuwa chanjo ya ugonjwa wa Covid-19 itakuwa na uwezo wa kutoa kinga kwa asilimia 50, lakini utengenezaji wa chanjo mpya umeonyesha kuwa chanjo hiyo itakuwa na uwezo wa kutoa kinga kwa zaidi ya asilimia 90.