Watu wengine 431 wameaga dunia kwa corona nchini Iran
Msemaji wa Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu ya Iran amesema kuwa, watu wengine zaidi ya elfu 12 wameambukizwa virusi vya corona na wengine 431 wamefariki dunia katika kipindi cha saa 24 zilizopita.
Bi Sima Sadat Lari ameeleza hayo leo wakati alipokuwa akitoa takwimu za karibuni kabisa za maambukizi ya corona hapa nchini na kuongeza kwamba, kwa mujibu wa matokeo ya vipimo rasmi walivyofanyiwa watu wenye maambukizi, katika muda wa masaa 24 yaliyopita wagonjwa wapya 12,931 waliokumbwa na ugonjwa wa COVID-19 wamegunduliwa humu nchini, ambapo 2,155 miongoni mwao wamelazwa hospitalini na waliobakia wamepatiwa huduma za tiba na kurudi nyumbani.
Aidha Dakta Lari amesema kuwa, idadi ya watu waliogunduliwa kupatwa na ugonjwa wa COVID-19 nchini Iran hadi hivi sasa imefikia 841,308 na kuongeza kuwa kufuatia wagonjwa 486 kuaga dunia katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita, jumla ya watu waliofariki dunia hadi sasa hapa nchini kutokana na ugonjwa huo imefikia 44,327.
Msemaji wa Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu ya Iran ameongeza kuwa hadi sasa watu 596,136 wamepona maradhi ya Covid-19 hapa nchini au wameruhusiwa kurudi nyumbani.
Wakati huo huo idadi ya watu walioambukizwa virusi vya corona duniani pia imepindukia milioni 58; ambapo kati ya hao watu wasiopungua milioni moja na 379,000 wameaga dunia na wengine zaidi ya milioni 40 wamepona.