Khatibzadeh: Misimamo ya Iran kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA haitabadilika
(last modified Mon, 07 Dec 2020 12:28:47 GMT )
Dec 07, 2020 12:28 UTC
  • Khatibzadeh: Misimamo ya Iran kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA haitabadilika

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa,misimamo ya Tehran kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA haitabadilika.

Saeed Khatibzadeh amesema hayo leo katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika kwa njia ya mawasiliano ya Intaneti ambapo akizungumzia matamshi ya Heiko Maas, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ujerumani kuhusu JCPOA amesema kuwa, mazungumzo kuhusu JCPOA yalishafika mara moja na kufikiwa makubaliano ya sasa ambayo yanaungwa mkono na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hivyo hakuna kitakachobadilika kuhusiana na kadhia hiyo.

Heiko Maas hivi karibuni aliamua kufuata mkumbo wa siasa za ikulu ya Marekani White House pale alipodai kwamba, eti kuna haja ya kuweko makubaliano ya juu zaidi na Iran ambayo yatadhamini maslahi ya Ulaya.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amebainisha kwamba, Ulaya inapaswa kufahamu na kudiriki nafasi na uwezo wake na kubainisha kwamba, madola ya Ulaya hayajatekeleza ahadi zake kwa mujibu wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

 

Khatibzadeh amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katu haitafanya mazungumzo na yeyote kuhusiana na usalama wake wa taifa na wala haina mpango kabisa wa kufanya mapatano katika hilo.

Kadhalika amesema kuwa, Iran inafahamu majukumu na haki zake na imezikumbusha pande nyingine kuhusiana na majukumu yao na kwamba,  kile ambacho hakikupatikana kupitia mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa bila shaka hakiwezi kupatikana kupitia njia nyingine.

Tags