Alkhamisi, tarehe 3 Oktoba, 2024
Leo ni Alkhamisi tarehe 29 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1446 Hijria sawa na Oktoba 3 mwaka 2024.
Siku kama ya leo miaka 158 iliyopita, wawakilishi wa Italia na utawala wa kifalme wa Austria walisaini Mkataba wa Vienna katika mji unaojulikana kwa jina hilo.
Kwa mujibu wa mkataba huo, Austria iliikabidhi Italia jimbo la Venice. Moja kati ya vipengee muhimu vya mkataba wa Vienna kilikuwa ni hiki kwamba, utawala wa kifalme wa Austria upigwe marufuku kuingilia masuala ya ndani ya Italia.
Mkataba wa Vienna ulifungua njia ya kuungana Italia mwaka 1870.
Miaka 92 iliyopita katika siku kama ya leo Iraq ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza.
Iran iliiweka Iraq chini ya mamlaka yake mwaka 539 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa (A.S). Iraq ilikuwa sehemu ya utawala wa kifalme wa Iran hadi ardhi hiyo ilipokombolewa na Waislamu mwaka 642 Miladia.
Iraq iliendelea kudhibitiwa na utawala huo wa kifalme hadi mwishoni mwa utawala wa Bani Ummayya na mji wa Baghdad ulichaguliwa kuwa makao makuu sambamba na kuingia madarakani utawala wa Bani Abbas.
Tarehe 3 Oktoba miaka 82 iliyopita kombora la kwanza lililotengenezwa na mwanadamu lilirushwa angani. Wernher von Braun alikuwa miongoni mwa wataalamu wa makombora wa Ujerumani ambao baada ya kuanza Vita vya Pili vya Dunia jeshi la nchi hiyo lilimpa jukumu la kutengeneza kombora la kwanza.
Tarehe 3 Oktoba mwaka 1942 kundi la wataalamu wa Ujerumani lilifanikiwa kurusha angani kombora hilo lililokuwa na urefu wa mita 14 na uzito wa karibu tani 13. Kombora hilo lilirushwa angani katika Bahari ya Baltic.
Miaka 80 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 29 Rabiul-Awwal, iliasisiwa taasisi ya kukurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu huko Cairo Misri.
Taasisi hiyo ilianzishwa kwa hima na juhudi kubwa za Muhammad Taqi Qomi mwakilishi wa Ayatullah Sayyid Hussein Tabatabai Boroujerdi, Marjaa Taqlidi katika zama hizo na Imamu wa al-Azhar Sheikh Muhammad Shaltut.
Watu kama Sayyid Jamal al-Ddin Asadabadi, mashuhuri kama Jamal Afghani, Sheikh Muhammad Abdu, Sheikh Muhammad Hussein Kashif al-Ghitaa na Sheikh Abdul-Majid Salim walijihusisha na kubadilisha mawazo na fikra katika uga huo.
Baada ya kuasisiwa taasisi hiyo ya kukurubisha maadhehebu zaa Kiislamu iliyojulikana kama Dar al-Taqrib Baina al-Madhahib al-Islamiyah" jarida la "Risalat al-Islam" nalo likaanza kuchapishwa. Jarida hili lilikuwa likichapisha makala za kielimu zenye thamani kuhusiana na madhehebu mbalimbali za Kiislamu.
Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, ilitangazwa rasmi habari ya kuungana tena Ujerumani ya Mashariki na Ujerumani ya Magharibi na nchi mbili hizo kwa mara nyingine tena zikaunda Ujerumani moja baada ya miaka 45 ya kutengana.
Baada ya kushindwa Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia, eneo la mashariki mwa Ujerumani lilikaliwa kwa mabavu na Urusi ya zamani na lile la magharibi likadhibiwa na nchi za Magharibi.
Nchi mbili za Ujerumani ya Magharibi na ya Mashariki zilitangazwa kuasisiwa mwaka 1949 kwa kuwa na mifumo miwili tafauti ya kisiasa na kiuchumi.