Watu wengine 134 waaga dunia kwa Covod-19 nchini Iran
Msemaji wa Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu ya Iran amesema kuwa, watu wengine zaidi ya elfu 5 wameambukizwa virusi vya corona na wengine 134 wamefariki dunia kwa Covid-19 katika kipindi cha saa 24 zilizopita.
Bi Sima Sadat Lari ameeleza hayo leo wakati akitoa takwimu za karibuni kabisa za maambukizi ya corona hapa nchini na kuongeza kwamba, kwa mujibu wa matokeo ya vipimo rasmi walivyofanyiwa watu katika muda wa masaa 24 yaliyopita wagonjwa wapya 5,760 waliokumbwa na ugonjwa wa COVID-19 wamegunduliwa humu nchini, ambapo 732 miongoni mwao wamelazwa hospitalini na waliobakia wamepatiwa huduma za tiba na kurudi nyumbani.
Aidha Dakta Lari amesema kuwa, idadi ya watu waliogunduliwa kupatwa na ugonjwa wa COVID-19 nchini Iran hadi hivi sasa imefikia 1,194,963 na kuongeza kuwa kufuatia wagonjwa 134 kuaga dunia katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita, jumla ya watu waliofariki dunia hadi sasa hapa nchini kutokana na ugonjwa huo imefikia 54,574.
Msemaji wa Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu ya Iran ameongeza kuwa hadi sasa watu 942,548 wamepona maradhi ya Covid-19 hapa nchini na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, vifo na maambuzi ya corona nchini Iran yameendelea kupungua katika siku za hivi karibuni kufuatia kanuni na sheria kali zinazotekelezwa na serikali ikishirikiana na Kamati ya Taifa ya Kupambana na Covid-19.
Katika uga wa kimataifa, Marekani imeendelea kuwa nchi iliyoathiriwa zaidi na corona ambapo karibu watu milioni 19 na laki tatu wameaambukizwa virusi hivyo huku zaidi ya laki tatu wakiwa wameaga dunia kwa Covid-19 nchini humo.