Zarif: Mauaji ya Hajj Qassem yanaonesha uchochole wa kupindukia wa Trump
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amegusia namna rais wa Marekani Donald Trump alivyotoa amri ya kuuliwa kiwogawoga, shahid Qassem Soleimani, na kusema kuwa, shambulio hilo la anga linaonesha uchochole wa kupindukia wa Donald Trump ambaye ameshindwa kupambana na shujaa huyo katika medani ya mapambano na badala yake alimvizia kiwogawoga uraiani na kumuua.
Shahid Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, aliuliwa kidhulma katika shambulio la kuvizia la anga lililofanywa na wanajeshi magaidi wa Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad, mji mkuu wa Iraq, tarehe 3 Januari, 2020 akiwa uraiani tena akiwa mgeni rasmi wa serikali ya Iraq, lakini Wamarekani hawakuheshimu hata protokali za kidiplomasia.
Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aidha amesema katika kipindi maalumu cha kumbukumbu ya mwaka mmoja ya kuuawa shahidi Hajj Qassem Soleimani ambacho kilirushwa hewani jana usiku na kanali ya tatu ya televisheni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba, Wamarekani walikuwa wanamuogopa kupindukia Hajj Qassem, walikuwa wanakiri kwamba alikuwa mtu wa kipekee katika medani za mapambano na ni kweli kwani shahid Soleimani alifanikiwa kufelisha njama za Wamarekani katika nchi za Syria, Iraq na Yemen.
Amesisitiza kuwa, hata katika medani ya kidiplomasia pia shahid Soleimani alikuwa mtu wa kipekee na kuongeza kuwa, Luteni Jenerali Soleimani hakuwa tu shujaa mkubwa wa mapambano dhidi ya ugaidi, bali alikuwa shujaa mkubwa pia katika jitihada za kupigania amani na usalama duniani.
Amezungumzia pia masuala ya Yemen na jinsi Saudi Arabia inavyopinga kupatikana amani katika nchi hiyo ya Kiarabu iliyoivamia na kuongeza kuwa, John Kerry, waziri wa mambo ya nje wa zamani wa Marekani mara tu baada ya kuanza uvamizi na uaudi wa Saudia nchini Yemen alisema, Wasaudia wanaamini kwamba watamaliza vita hivyo katika kipindi cha wiki tatu tu, lakini wiki hizo tatu sasa zimeingia katika mwaka wa sita na bado vita vinaendelea.