Jan 15, 2021 14:49 UTC
  • Iran: Saudia imegeuka wakala wa kutekeleza mipango ghalati ya Israel

Msaidizi maalumu wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa amesema watawala wa Saudi Arabia wamegeuka na kuwa wakala wa kutekeleza sera na mipango ghalati ya utawala haramu wa Israel katika eneo la Asia Magharibi.

Hussein Amir-Abdollahian amesema hayo katika radiamali yake kwa matamshi ya kipropaganda yaliyotolewa hivi karibuni na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa, badala ya utawala wa Riyadh kukariri madai yake yasiyo na msingi dhidi ya Tehran, ni bora uhitimishe sera zake za kuchochea moto wa vita, kushajiisha ugaidi na kuchangia vikwazo dhidi ya mataifa mbalimbali.

Ameeleza bayana kuwa, uungaji mkono wa moja kwa moja na usio wa moja kwa moja wa Riyadh kwa magenge ya kigaidi likiwemo kundi la ISIS ni jambo ambalo limethibitishwa kwa miaka mingi, hususan na watu wa mataifa ya Iraq na Syria. 

Amir-Abdollahian amewaasa watawala wa Riyadh kutazama upya sera zao za kigeni zilizojaa uhasama, na badala yake waanze kuchukua hatua ya kuwa na uhusiano wenye manufaa, wa kirafiki na kidugu na majirani zao katika eneo.  

Sehemu ya mashambulizi ya Saudia dhidi ya Yemen

Jana Alkhamisi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Saudia, Faisal bin Farhan aliwaambia waandishi wa habari akiwa pamoja na mwenzake wa Russia Sergei Lavorv mjini Moscow kuwa, uwepo wa Iran nchini Syria unazuia kupatikana suluhu katika mgogoro unaoikabili nchi hiyo ya Kiarabu.

Msaidizi maalumu wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa ameitaka Saudia kabla ya kubwabwaja na kuibua tuhuma bandia dhidi ya Iran, isitishe vita dhidi ya taifa la Yemen na mauaji ya halaiki ya wanawake na watoto wa nchi hiyo maskini jirani yake.

 

Tags