Iran yajibu bwabwaja za Ufaransa juu ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA
(last modified Sun, 31 Jan 2021 03:26:01 GMT )
Jan 31, 2021 03:26 UTC
  • Iran yajibu bwabwaja za Ufaransa juu ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema silaha za Ufaransa na nchi nyingine za Magharibi ndilo chimbuko kuu la ukosefu wa uthabiti katika eneo la Ghuba ya Uajemi.

Saeed Khatibzadeh alisema hayo jana Jumamosi na kuongeza kuwa, madhali Ufaransa, Uingereza, Marekani na nchi nyinginezo zinaendelea kurundika silaha katika eneo hili, basi ukosefu wa usalama na uthabiti utaendelea kushuhudiwa.

Kauli ya Khatibzadeh ni jibu kwa matamshi ya Ijumaa ya Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron aliyedai kuwa, mazungumzo yoyote mapya kuhusu makubaliano ya nyuklia ya Iran ya JCPOA yanapaswa kujumuisha waitifaki wa Ufaransa katika eneo la Asia Maghairibi, kama vile Saudi Arabia.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ameeleza bayana kuwa, JCPOA ni mapatano ya kimataifa na kamwe hayawezi kujadiliwa upya wala kujumuisha wadau wapya.

Ameitaka serikali ya Paris badala ya kubwabwaja, itazame upya sera zake za kigeni na iache kurundika silaha katika eneo hili la Asia Magharibi.

Rais Macron wa Ufaransa

Khatibzadeh ameashiria hatua ya Marekani ya kujiondoa katika JCPOA na kubainisha kuwa, Washington ilijitoa kwenye mapatano hayo ya kimataifa huku Ulaya ikishindwa kuyalinda; na iwapo kuna chembe ya matumaini ya kuhuisha makubaliano hayo, njia ya kufuata ni rahisi na sahali.

Ameongeza kuwa, Marekani inapaswa kurejea katika mapatano hayo pasi na masharti yoyote, sambamba na kuliondolea taifa hili vikwazo vinavyofungamana na JCPOA na visivyofungamana nayo, vilivyowekwa na aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Donald Trump.  

 

Tags