Mjumbe Maalumu wa UN nchini Yemen afanya mazungumzo na mshauri wa Zarif
Mjumbe Malumu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Yemen amefanya mazungumzo na mshauri maalumu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ambapo wamejadili matukio ya hivi karibuni ya Yemen.
Kwa mujibu wa taarifa, Ali Asghar Khaji, ambaye ni mshauri mwandamizi wa masuala ya kisiasa wa Mohammad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekutana na kufanya mazungumzo na Martin Griffiths, Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen. Katika mkutano huo uliofanyika hapa mjini Tehran Jumapili, wawili hao wamejadili masuala mbali mbali yanayohusiana na mgogoro wa Yemen. Aidha wamejadili njia za usitishwaji vita nchini humo.
Katika kikao hicho, Khaji ameashiria hali mbaya sana ya watu wa Yemen wanaokumbwa na masaibu na hali ngumu ya maisha kutokana na vita vya kulazimishwa na pia mzingirio wa kidhalimu wa kiuchumi. Mwanadiplomasia huyo wa Iran ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuingilia kati ili vita dhidi ya Yemen visitishwe mara moja sambamba na kuondolewa mzingiro usio wa kibinadamu dhidi ya nchi hiyo.
Aidha ametangaza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kutoa misaada ya kibinadamu na kitiba kwa watu wa Yemen katika kukabiliana na corona. Hali kadhalika Khaji amesisitiza ulazima wa kutatuliwa mgogoro wa Yemen kupitia mazungumzo ya Wayemen kwa Wayemen sambamba na kuundwa serikali jumuishi.
Kwa upande wake Martin Griffiths, Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina nafasi muhimu katika mchakato wa amani ya Yemen na eneo zima. Amesema Umoja wa Mataifa unajitahidi kuhakikisha kuwa kunafikiwa mapatano ya usitishwaji vita Yemen sambamba na kuondolewa mzingiro wa kiuchumi na hali kadhalika kuanzishwa tena mazungumzo ya kisiasa.
Ikumbukwe kuwa mnamo mwezi Machi 2015 Saudi Arabia, ikiungwa mkono na Marekani, utawala haramu wa Israel, Umoja wa Falme za Kiarabu na nchi zingine kadhaa iliivamia kijeshi Yemen na kuiwekea mzingiro wa kila upande.
Utawala dhalimu wa Saudia ulianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha madarakani kibaraka wake, Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh. Hata hivyo hadi sasa Saudia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao kutokana na kusimama kidete wananchi wa Yemen.
Hivi karibuni, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lilisema kati ya Januari na Juni 2021, asilimia 54 ya Wayemen, yaani watu milioni 16.2, watakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.
Aidha mwezi Disemba mwaka jana, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilitangaza kuwa vita vya Saudi Arabia dhidi ya Yemen vimepelekea zaidi ya watu 233,000 kupoteza maisha katika kipindi cha miaka sita iliyopita.