"Mlango wa fursa kwa Marekani kurekebisha makosa ya Trump unakaribia kujifunga"
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amesema iwapo Marekani na nchi za Ulaya zitaendelea kujikokota katika utekelezaji na kufungamana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, basi Jamhuri ya Kiislamu karibuni hivi itachukua hatua nyingine mpya za kupunguza uwajibikaji wake katika mapatano hayo.
Muhammad Javad Zarif alisema hayo jana Jumatano kwa mnasaba wa maadhimisho ya mwaka wa 42 wa Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa, utawala mpya wa Marekani wa Joe Biden unapaswa kuirejesha Washington katika mapatano hayo, na kwamba mlango wa fursa hiyo unakaribia kujifunga kwa kasi kubwa.
Amesema utawala wa sasa wa Marekani unapaswa kujifunza kutokana na mapungufu na kasoro za utawala uliopita wa Donald Trump, vinginevyo utapata hatima sawa na ya mtangulizi huyo wa Biden.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameeleza bayana kuwa, hatua mpya zitakazochukuliwa na Iran kama zilivyodhinishwa na Bunge la Iran na katika fremu ya makubaliano ya JCPOA zitajumuisha kupanua miradi ya nyuklia ya Iran na kupunguza ushirikiano na waangalizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).
Dakta Zarif amesisitiza kuwa, Iran haijaondoka katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA bali imepunguza utekelezaji wa baadhi ya vipengee vyake kwa kufuata miongozo iliyoanishwa kwenye makubaliano hayo ya kimataifa.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameongeza kuwa, lengo kuu la Jamhuri ya Kiislamu katika jitihada zote hizo ni kuunda eneo ambalo lina usalama, ustawi na uthabiti zaidi.