Araqchi: JCPOA haina maana yoyote iwapo vikwazo dhidi ya Iran havitaondolewa
(last modified Sat, 13 Feb 2021 08:40:45 GMT )
Feb 13, 2021 08:40 UTC
  • Araqchi: JCPOA haina maana yoyote iwapo vikwazo dhidi ya Iran havitaondolewa

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa amesema makubaliano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA hayatakuwa na maana wala thamani yoyote iwapo vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu havitaondolewa.

Sayyid Abbas Araqchi amesema hayo leo Jumamosi katika mahojiano na tovuti ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kubainisha kuwa, kwa mujibu wa JCPOA, Iran inapaswa kuondolewa vikwazo vyote vikiwemo ilivyowekewa baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano hayo na ilivyowekewa kwa kutumia hadaa za kisheria.

Ameeleza bayana kuwa, JCPOA imejengeka katika misingi miwili mikuu; mosi ni mienendo ya miradi ya nyuklia ya Iran kwa muda maalumu, na pili vikwazo dhidi ya Iran ambavyo upande wa pili unapaswa kuviondoa.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amefafanua kuwa, iwapo misingi hiyo miwili itakosekana, basi mapatano hayo ya kimataifa ya nyuklia hayatakuwa na mantiki yoyote.

Bendera za nchi washiriki wa JCPOA

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa ameshiria kuhusu azma ya Marekani ya kurejea katika JCPOA na kusisitiza kuwa, jambo la muhimu kwa taifa la Iran ni iwapo kurejea huko kutapelekea kufutwa vikwazo hivyo vya kidhalimu.

Ameongeza kuwa, kinachofanywa hivi sasa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kupunguza uwajibikaji wake kwenye mapatano hayo ni radimali kwa hatua ya upande mmoja ya Marekani ya kujiondoa kwenye makubaliano hayo kinyume cha sheria.

 

Tags