Feb 13, 2021 11:21 UTC
  • Rouhani: Kuielewa Qurani Tukufu, ndio ufunguo wa kuongoka vijana

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuyaelewa mafundisho sahihi ya Qurani Tukufu ndio ufunguo wa kuongoka katika njia iliyonyooka tabaka la vijana.

Rais Rouhani amesema hayo leo Jumamosi katika hafla ya kuwaenzi wahudumu wa Qurani Tukufu na kuongeza kuwa, kizazi cha vijana kitaongoka iwapo kitafuata vizuri na kuyaelewa mafundisho sahihi na miongozo ya kitabu hicho kitakatifu cha Waislamu.

Kadhalika Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekumbusha kuwa, "Rajab na Shaaban ni miezi miwili inayotuandaa kuupokea mwezi mtukufu wa baraka wa Ramadhani." Leo Jumamosi imesadifiana na tarehe Mosi Rajab, mwezi uliojaa rehema na fadhila tele. 

Amebainisha kuwa, "Allah hutupa uongofu katika miezi ya Rajab na Shaaban ili tuweze kujiandaa kwa saum (funga) na qiyam (visimamo vya ibada)."

Dakta Rouhani ameendelea kuuasa Umma wa Kiislamu kwa kuuambia kuwa, waumini wa Kiislamu wanapaswa kuzidhibiti ndimi zao na kuchunga matamshi yao. Pia wanapaswa kuisoma Qurani Tukufu kwa sauti nzuri kwani kufanya hivyo ni sawa na kutumia lugha kwa ufasaha.

Qurani Tukufu

Wakati huohuo, Rais Hassan Rouhani katika hotuba yake mapema leo katika Makao Makuu ya Jopokazi la Kupambana na Corona hapa mjini Tehran ametoa mwito wa kuchungwa protokali za mipaka ili kuhakikisha kuwa spishi mpya za virusi vya corona haziingii nchini hapa. 

Amesema wasafiri wote wanaokuja hapa nchini wanatazamiwa kuzingatia protokali za kitaifa na kimataifa za afya ama katika kufanyiwa vipimo au kuwekwa karantini.

Tags