Rais Rouhani: Iran haina mpango wa kutumia silaha za maangamizi ya umati
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i66952-rais_rouhani_iran_haina_mpango_wa_kutumia_silaha_za_maangamizi_ya_umati
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema nchi hii haijawahi kuwa na mpango wa kumiliki silaha za nyuklia wala kuzitumia.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 17, 2021 08:07 UTC
  • Rais Rouhani: Iran haina mpango wa kutumia silaha za maangamizi ya umati

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema nchi hii haijawahi kuwa na mpango wa kumiliki silaha za nyuklia wala kuzitumia.

Akizungumza Jumatano katika kikao cha baraza la mawaziri, Rais Rouhani amesema: "Kama ambavyo tumesema mara kadhaa, silaha za maangamizi ya umati, zikiwemo silaha za nyuklia, hazina nafasi yoyote katika mpango wa nchi hii wa kiulinzi na huu ndio msimamo thabiti wa Jamhuri ya Kiislamu.

Rais Rouhani hata hivyo amesisitiza kuwa, Iran itaendelea kufuatilia teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani kwani hiyo ni haki yake.

Aidha amesema Iran ni mwanachama wa mkataba wa NPT wa kuzuia uundwaji na usambazwaji silaha za nyuklia na pia inashirikiana na Wakala wa Kimataifa wa Atomiki IAEA na imetekeleza maagizo ya wakala huo kuhusiana na usalama wa kinyuklia.

Rais Rouhani amesema Iran haina mpango wa siri wa nyuklia na kuongeza kuwa Iran haijawahi kuwa na mpango kama huo na huo ni uamuzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ameongeza kuwa, hata dunia nzima ikisema silaha za nyuklia ni nzuri kwa Iran, msimamo wa Iran hautabadilika.

Ameongeza kuwa, "Mtazamo wetu umetangazwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kama Fatuwa. Msimamo huo ndio ambao tumeutia saini katika mkataba wa NPT na hatutavunja mkataba huo."