Iran: Muhula wa kusimamisha 'Protokali ya Ziada' unakaelekea kumalizika
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa ameonya kuwa, iwapo Marekani haitachukua hatua yoyote ya kuliondolea vikwazo taifa hili kufikia kesho kutwa (Februar 23), basi Tehran itachukua hatua ya kusimamisha Protokali ya Ziada ya kupunguza kiwango cha uangalizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).
Sayyid Abbas Araqchi alisema hayo jana usiku katika mahojiano yaliyorushwa hewani na kanali moja ya hapa nchini na kuongeza kuwa, moja ya nara zilizotumiwa na Joe Biden katika kampeni zake za uchaguzi wa rais wa Marekani ilikuwa kuirejesha Washington katika JCPOA. Makubaliano hayo yalikuwa mafanikio makubwa kwa Wademocrats, na ni kwa maslahi yao wenyewe kurejea kwayo. Sera ya Donald Trump ya mashinikizo ya juu kabisa imefeli, na inapaswa kubadilishwa.
Ameeleza bayana kuwa, kupunguza kiwango cha uangalizi wa IAEA hakuna maana ya kusimamisha kikamilifu uangalizi huo, na kwamba hatua hiyo itachukuliwa kwa mujibu wa sheria iliyopitishwa na Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran).
Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran limeshaitangazia rasmi IAEA kwamba, kuanzia tarehe 23 Februari, hatua zilizochukuliwa kwa khiari na Iran za kutekeleza itifaki ya ziada zitasimamishwa, lakini uangalizi wa wakala huo wa atomiki utaendelea.
Sayyid Araqchi amebainisha kuwa, Iran inatafakari ombi la Umoja wa Ulaya la kuwa mwenyeji wa mkutano usio rasmi baina ya Tehran na washirika wengine wa mapatano ya nyuklia ya JCPOA, ambapo Washington imeomba pia kuushiriki kama mgeni.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amekumbusha kuwa, makubaliano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA hayatakuwa na maana iwapo vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu havitaondolewa.